Kesho Ya Manyani - Hadithi Ya Maamuzi
Kesho Ya Manyani
Kesho Ya Manyani Hadithi Inayotufunza Kuhusu Maamuzi
Mvua ilinyesha kwa nguvu, kama vile mawingu yalikuwa yamemimina mapipa ya maji moja kwa moja kutoka angani. Manyani walihangaika kila mmoja akitafuta mahali pa kujificha na kuwalinda watoto wake dhidi ya mvua kali. Lakini juhudi zao zilionekana kugonga mwamba. Hakukuwa na mahali pa uhakika, kila mmoja akihangaika kwa njia yake.
Katika kipindi cha jua kali, maisha yao hayakuwa na changamoto kubwa. Walistarehe kwenye miti, wakicheza na kula kwa amani. Lakini kila mvua iliponyesha, hali ilikuwa tofauti-baridi, mvua kubwa, na usumbufu usio wa kawaida.
Siku moja, manyani walijadiliana:
"Hili haliwezi kuendelea! Inabidi tujenge makazi ya kudumu. Tunateseka kila mwaka, wakati binadamu hawahangaiki kama sisi."
Mmoja akaongeza “Kesho nitakwenda mwituni, nitakata miti, nitajenga nyumba yangu!"
Lakini mvua ilipokwisha, hali ikarejea kama kawaida. Manyani wakasahau mateso yao. Walirudia maisha ya kawaida-wakicheza, wakila, na kusahau ahadi yao. Ilikuwa ni hadithi ileile, kizazi baada ya kizazi. Mababu zao walikuwa na wazo hilo hilo la kujenga makazi, lakini hakuna aliyewahi kulitekeleza.
Msemo "Kesho ya manyani" ukaziwa-kesho ambayo haijawahi kufika.
Tunajifunza Nini Kupitia Manyani?
Ukweli ni kwamba, sisi binadamu mara nyingi tunafanya mambo yanayofanana na manyani hawa. Tunajua tunachotakiwa kufanya ili kuboresha maisha yetu, lakini tunaahirisha kila siku.
Umesema utaanza kuweka akiba kesho?
Umesema utaanza biashara yako kesho?
Umesema utaanza kusoma kitabu fulani kesho?
Umesema utaanza kufanya mazoezi kesho?
Lakini kesho hiyo haijafika na labda haitawahi kufika!
Kila dakika inayopita haitarudi tena. Kila siku mpya inakuja na changamoto zake, na ukizidi kuahirisha mambo, utajikuta unajenga mlima wa majukumu yasiyotimizwa. Hatimaye, ndoto zako zitazimika kwa sababu tu hukuchukua hatua kwa wakati.
Jambo La Kufanya!
Badala ya kusema "Kesho nitafanya," anza sasa hivi! Chukua hatua ndogo leo. Kama ni biashara, tafuta taarifa leo. Kama ni kuweka akiba, anza na hata kiasi kidogo. Kama ni afya yako, tembea hata kwa dakika kumi leo.
Maisha hayangoji. Wale wanaoendelea mbele si kwa sababu wanajua kila kitu, bali kwa sababu waliamua kuanza-na wakaanza mara moja!
Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Kama kuna namna unafika mahali hujui mahali pa kuanzia ili uweze kupata kutambua kusudi la kuwepo hapa duniani basi tunakukaribisha tuwasiliane tutakusaidia. Bofya mahali palipoandikwa "USHAURI NA MAFUNZO BOFYA HAPA" nasi tutakufikia mapema.
Ningependa kusikia maoni yako! Unaweza kuwasiliana nami kwa WhatsApp, ujumbe mfupi wa maneno, au simu kwa namba yangu hapa chini.
Ni mimi, rafiki na kocha wako, Philipo Lulale
WhatsApp: +255 784 503 076
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com