Maneno Huumba!
MANENO HUUMBA
“Mungu hukupa kile unachoomba” Umewahi kusikia huu msemo ukitumiwa na watu wengi? Ni vigumu kujua kama watu wengi wanaotumia hii misemo wanaujua ukweli na maana yake au wanaitumia tu kwa sababu imezoeleka katika jamii!
Naamini umewahi kuitumia hata wewe mwenyewe binafsi.Mimi nimeitumia misemo ya aina hii mara nyingi kabla sijajua hata hesabu yake sikumbuki.Tangu nijue maana na uzito wa maneno ninahakikisha kwamba nakuwa mwangalifu sana kwa maneno ninayojisemea mwenyewe na wanayonisemea watu.Kwa kifupi nachagua nini cha kujisemea na nini nisijisemee.
Sina uhakika kama watu wengi wanajua uzito,nguvu na madhara ya misemo wanayojisemea kila siku na kukubali watu wanavyowasemea.Maneno tunayojitamkia na kukiri kwa vinywa vyetu kila siku nataka nikwambie yana nguvu kubwa ya kuumba.
Pengine ninapongea na wewe hapa inawezekana unashangaa ni maneno gani haya anayojaribu kutueleza hapa.Ngoja nifafanue unayajua kabisa:kama wewe ukiamka asubuhi kazi ya kwanza kinywani mwako ni kukiri tu jinsi usivyoweza kufanya jambo fulani basi hayo ni maandalizi ya kupata kile unachokiri hivyo uwe tayari kupokea.
Kitu cha muhimu hapa kukumbuka siku zote ni kwamba mwanadamu umeumbwa kwa upendeleo mkubwa na hakuna kiumbe kingine chochote kilichopendelewa kama wewe.Kwa hiyo ndani mwako umewekwa uwezo wa ajabu wa kubuni na kufanya chochote unachotaka kufanya bila kujali hali yako. Ukibaini ukweli huo basi utakuwa mwangalifu sana juu ya maneno unayosema na kuwasemea watu wengine,kwa nini?
Kuna makundi mawili ya maneno haya yanayosemwa:yale tunayojisemea wenyewe na yale watu wanayotusemea.
1.MANENO TUNAYOJISEMEA
Haya ni maneno mepesi tunayojisemea kila siku kwa kujua au hata bila kujua.Kama kila siku kazi yako ni kujisemea kuwa huwezi kufanya jambo lolote kwa kuwa huna uwezo nalo,basi uwe tayari kupokea unachokiri kwa sababu umejiandaa kupokea unachokiri.Kumbuka kitu hicho hicho unachohalalisha kwamba huwezi kukifanya kwa visingizio unavyo viita sababu,jirani yako kuna mtu anakifanya kwa mafanikio makubwa na wala hakuwa na uwezo ulio nao wewe.
Utakuta mwanafunzi darasani yeye kazi yake ni kukiri kushindwa na ameshatengeneza uhalali wa kile anachoamini kutokea katika maisha yake,basi hatakaa awe mwanafunzi bora hata siku moja,lakini kwa nini uwe mtazamaji!
Kama akilini mwako unajiona kila skiu kipato chako ni kidogo hutaweza kujenga nyumba,kununua gari,kusomesha watoto shule nzuri,kula vizuri,kusaidia watu wengine maishani mwako basi ndivyo itakavyokuwa kwako.Kumbuka watu hawafanyi vitu kwa kuwa wana pesa nyingi bali wanafanya kwa sababu wana moyo wa kufanya hivyo na nguvu kufuatilia ndoto zao.
Kama pesa ingekuwa ndicho kigezo pekee cha kuwezesha mtu kufanya vitu wanaoshinda michezo ya kubahatisha na wachezaji maarufu duniani wangekuwa na maendeleo makubwa.
Ni muhimu kubadilika na kuanza kuchagua maneno ya kuwasemea watu wengine lakini unapaswa kuanza kubadilika wewe binafsi kwanza kabla ya kuanza kushughulikia watu wengine. Kama kuna maneno ya kuogopa kati ya makundi haya mawili,basi ni yale maneno ambayo mtu anajisemea mwenyewe kila siku.Haya ndiyo yanayoweza kuua hata nafsi ya mtu mwenyewe kuliko yale maneno unayosemewa na watu wengine.
Mara nyingi hatuishi kwa kutegemea mawazo au maneno ya watu wanavyosema la hasha.Mtu akikusema kwamba wewe huwezi kufanya kitu chochote kwa kigezo cha hali yako au historia ya uliko toka;huna haja kugombana naye badala yake fanya mpaka uthibitishe kwamba yeye ni mwongo.Vinginevyo ukichagua kuamini alivyosema utawajibika kwa matokeo yako mwenyewe.
MANENO YA KUSEMEWA NA WATU WENGINE
Wakati mwingine tumesemewa na watu wengine maneno magumu na kujikuta tunaridhika na kukubali kuishi maneno ya watu kwa kufuatana na jinsi dunia inavyoamua kwa sababu hatuujui ukweli wa mambo katika eneo hili.Utakuta mtu anakwambia wewe huwezi kufanya jambo hili huna pesa,na wewe huwezi kushindana na fulani,wewe huwezi hili,huwezi lile na bahati mbaya na wewe unakubaliana na hukumu ya dunia unanyoosha mikono kukiri kushindwa.
Maneno ya aina hii tumetamkiwa na kutamkia watu wa mbali na wale walio karibu na sisi kama watoto wetu,waume zetu,wake zetu na matokeo yake kile tunachoamini na kutamka mara kwa mara kinakuwa na uhalali wa kuishi,halafu tunaanza kulaumu na kulalamika.
Kitu cha msingi kujua ni kwamba kwa kuwa tunaishi na watu lazima tutegemee kusimia mawazo mchanganyiko kutoka kwao.Mtu anaweza kudhibiti mawazo yake lakini hawezi kudhibiti mawazo ya mtu mwingine.Ni kupoteza muda kujaribu kutumia muda wako kudhibiti mawazo na maneno ya watu wengini,badala yake tutumie muda kudhibiti maneno ya vinywa vyetu tunayojiambia nay ale tunayoambia watu wengine.
Tuepuke sana wazazi kwa mfano kuambia watoto huna akili,wewe malaya,wewe mbwa,wewe huwezi hili,awe mwanao au wa mwenzio usifanye kabisa madhara yake ni makubwa.
Unajua kama una kawaida ya kumsalimia mwanao kwa kumwita wewe mbwa njoo,maana yake kichwani mwa mtoto itaanza kujengeka picha ya mbwa kwa sababu watoto wanaamini wazazi wao kuwa ndio makocha wa kila kitu,hivyo ataanza kufanya tabia za kiumbwa mbwa baadaye utalia utakapokuja kukumbuka umekwishachelewa.
Mara nyingi nimekutana na watu wanaonifahamu vizuri na wanajua nafanya kazi lakini katika maneno ya kusalimia wanachanganya na swali la “habari za kuhangaika?” Kabla hatujaendelea mimi huwa nakanusha kwamba mimi kwa kweli sihangaiki ila nafanya kazi na Mungu ananibariki naendesha maisha yangu na familia.Huwa wanabaki wakicheka huku mimi nikiwa nimewarudishia maneno yao wayamiliki wenyewe.Kufanya kazi ni kitu kingine na kuhangaika ni kitu kingine na mimi sitaki kuhangaika nafanya kazi.
Kile unachojisemea au unachojitabiria ndicho ambacho utapata katika maisha yako,kwa hiyo unahitaji kuwa mwangalifu sana na kwa kweli kuchagua maneno ya kusemea watu wengine na yale unayojisemea mwenyewe.
Maneno hayo ndiyo yanayotuumba kwa kujenga hata kutubomoa kabisa katika maisha yetu.
Mimi na wewe tunao uwezo wa kuzuia maneno hasi tunayojisemea wenyewe ili kuruhusu tu maneno yanayoleta nguvu maishani mwetu.Hebu tupangue kila neno hasi linalosemwa na watu kwetu na watu wengine kwa sababu Unachokiri ndicho unachoishi.
Naamini kuna kitu cha kukusaidia utakuwa umepata kwenye makala hii fupi.Kama ungependa kuwasiliana kwa ushauri au ngependa kuingia zaidi kwa undani kwenye mada hizi,basi usisite kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno,whatsap au kupiga kwa no
Ni mimi mtumishi wako na kocha Philipo Lulale
WhatsApp +255784503076
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com