MIMI Naitwa Muda Mnitumie Vizuri!
Muda una thamani kuliko pesa
Mimi naitwa MUDA,ndio naitwa Muda ndilo jina langu.Nimesubiri kutambulishwa leo nimechoka kusubiri nimeamua kuvunja huo mwiko najitambulisha mwenyewe mimi naitwa Muda. Kutokunifahamu vizuri kumesababisha mkanganyiko na majuto makubwa kwa wanadamu wengi. +160#
Kwa nini nimeamua kujitambulisha mwenyewe badala ya kuendelea kusubiri kutambulishwa? Ni kwa sababu watu wengi wala hawajali kunitambulisha kuwa kama kitu cha muhimu kwa sababu hawajui umuhimu wangu katika maisha.
Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “MIMI NAITWA MUDA.” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana.
Bahati mbaya sana hata wale wanaonitambulisha wengi wao wananitambulisha kimakosa cha ajabu hata wale marafiki zangu wa karibu wanakosea kunitambulisha. Nakwambia kama marafiki ingekuwa ni mtaji ninao marafiki wengi kila kona duniani,lakini hata wanaodai kunifahamu vizuri inapofika wakati wa kunitambulisha wananikosea! Na hiki ndicho kilichonisukuma leo kujitamulisha mwenyewe.
Wakati mwingine inabidi uingilie kati ili kujitambulisha sahihi mwenyewe. Siyo kwamba najisifu hapana nataka kukuambia tu kwamba mimi ni mtu muhimu sana katika maisha ya kila kitu wala silingani wala kufanana kwa sifa na vitu vingi ambavyo mnanifananisha navyo.
Hebu tafakari ni nani miongoni mwenu ambaye hanihitaji unadhani? Hakuna! Watawala na watawaliwa wananihitaji,matajiri na maskini wananihitaji bila kujali hali wala mipaka yao ya kijiografia na uwezo wao kiuchumi.Nina thamani kubwa ingawa watu wengi wananidharau kwa sababu hawanijui na wakati mwingine hali yangu ya ukimya inafanya wanichukulie wanavyotaka. Bila mimi hakuna ambacho kingefanyika,wala ambacho kinafatanyika hata hakuna ambacho kitafanyika.
KIla mtu ananihitaji bila kujali hali wala chochote sina ubaguzi,kinyongo wala hasira. Maskini ananihitaji,tajiri anahitaji,wanawake na wanaume wananihitaji,watoto na wakubwa wananihitaji.Sina ubaguzi hata kidogo wote ninawahudumia kwa usawa bila upendeleo wa aina yoyote. Mimi ninahitajika kuliko ninavyowahitaji nyinyi.
Afrika wananihitaji,Amerika wananihitaji,Asia wananihitaji,Australia wananihitaji,hakuna asiyenihitaji hata mmoja wote wananihitaji kulingana na umuhimu wangu. Angalia mkisherehekea mnanihitaji,mkiomboleza mnanihitaji.Mkirejea kumbukumbu zenu za matukio yaliyopita mnanihitaji pia.
Mimi ndiye ninaye weka viwango katika maisha ya mwanadamu tofauti kati wa wadogo na wakubwa,waliofanikiwa na wasiofanikiwa,walionitumia vizuri na wale ambao hawakunitumia vizuri,wale wanaojuta na wale wanaofurahia uwepo wao hapa duniani.Wale ambao maisha yao yanagusa maisha ya watu wengine na ambao maisha yao hayana madhara yoyote kwa maisha ya watu wengine.Mimi naitwa MUDA jamani.
Licha ya umuhimu wangu kama nilivyojaribu kujitambulisha kwa ufasaha hapo juu,ninayo majonzi makubwa kwani miongoni mwa vitu ambavyo havieleweki na binadamu wengi, basi ni mimi. Hebu tazama vitu vingine vyote wanavyovitazama halafu uangalie mimi wanavyonichukulia utachoka.
Ukitokea upungufu katika idara,kitengo au maisha yoyote ya mtu basi wa kwanza kufikiriwa kufujwa ni mimi bila hata kufikiria madhara ya mbele ya kufanya hivyo,lakini mimi siachi kuachilia upendo juu yao bado nawapenda tu.Nawapenda hata kama watu hawanijali silipi baya kwa ukbaya ila naachilia wema siku zote mimi naachiliwa wema kwa watu wakati natimiza wajibu wangu niliopewa na Mungu.
Wengine wanalazimisha kunilinganisha mimi na fedha lakini angalia heshima wanayompa fedha na mimi tofauti.Hata hivyo mimi siyo fedha mimi ni muda jamani tena nilkuwepo kabla hata ya fedha haijakuwepo hapa duniani.Mimi ni mtangulizi wa kila kitu hata pesa kabla haijakuwepo mimi nilikuwepo! Sasa mnaanzia wapi kunilinganisha na watoto wadogo wa Judi kama pesa?. Nilikuwepo,nipo na nitakuwepo.KIla kitu kitaniacha hapa.
Wengine wanataka kunifananisha na dhahabu,wengine almasi wengine wananifananisha na vito vya thamani,hapana mimi ni muda jamani nilikuwepo kabla ya hivyo mnavyoona vya thamani kuwepo.Mimi ni miongoni mwa waanzilishi wa sayari yetu. Pesa,dhahabu,almasi, tanzanite mbona hao ni watoto wa juzi walizaliwa mimi nawaona tayari nikiwa mtu mzima? siwezi kufanana nao kwa umri wala thamani mimi ni kitu cha thamani jamani na nimekula miaka mini hapa duniani.
Naona unaanza kukasirika eti ninatumia muda mwingi! Hapana ngoja nimalizie kwa kusisitiza tena kipengere muhimu hapa halafu nigeuke na kukuacha huku nakiwa nimetimiza dajibu wangu kwako. Mimi ni muda jamani,ndiye ninayetenganisha watu katika makundi,watoto,vijana na wazee,waliofanikiwa na wale wasiofanikiwa kutegemeana na namna mtu alivyonichukulia.
Ukisikia mtu anaitwa mtoto maana yake yeye hajatumia muda mwingi,kijana yeye yuko katikati ya anakokwenda na kule anakotoka,lakini ukisikia mtu anaitwa mzee maana yake mtu huyo amekwishatumia muda wake mwingi kuliko muda uliobaki.Kama kuna mambo ambayo hakufanya kipindi akiwa kijana,jamani mimi naitwa muda,sijui kama unanielewa.
Mimi huwezi kunilinganisha na pesa kama ambavyo mmekuwa mkitumia misemo ya kupotosha eti muda ni mali (pesa) mimi ni zaidi ya pesa ingawa mara nyingi mmekuwa mkidai eti thamani yangu ni kama pesa.Lakini angalia hata kwa hiyo misemo ya watu namna ambavyo hamnitendei haki angalia manavyonichukulia. Kama ningekuwa tu na thamani kama pesa mbona basi pesa mnatungia bajeti lakini muda hamna nafasi ya kufanya bajeti? Si mnajua mnavyonitumia hovyo!
Kama mnajali mbona siioni nidhamu kwenu kwamba kweli mnanithamini? Kwa nini nasema mimi ni zaidi ya pesa? Pesa unaweza kupoteza ukaipata tena lakini mimi muda ukinipoteza hakuna namna utafanya kuweza kunirudisha nikitoka nimetoka.
Walionijali na kunitumia vizuri wamefanikiwa sana katika maisha yao wamefanya vitu vya kugusa maisha ya watu wengine na wale walionipuuza wanamaliza maisha yao kwa majuto makubwa sana, huku wakitamani siku zirudi nyuma wajaribu kurekebisha makosa ya nyuma lakini, mimi ni muda nikitoka nimetoka.
Nataka kukusihi tu kwamba mimi nina nguvu kubwa ninakuzidi kwa mambo mengi,kama ninakuzidi naomba ufanye kama wengine waliofanikiwa walivyofanya tafuta njia,fanya vyoyote utakavyofanya ushirikiane na mimi,nami nakuhakikishia utafanikiwa sana. Naitwa muda jamani niko kama ukuta ukishindana nami utaumia.
Ngoja nimtambulishe rafiki yangu wa karibu kwako anaitwa “MABADILIKO” sisi tukiingia mahali hakuna wa kutuzuia lazima tufanye yale tunayotaka kufanya. Ni sisi tunaosababisha watu waonekane ni watoto,vijana na pia wazee. Cha ajabu watu wengi hawajui kama sisi ni watu muhimu wanatuchukulia rahisi tu!
Watu wengi wanachanganya kwamba eti mimi nina kawaida ya kwisha hapana! Mimi sina mwisho isipokuwa wateja wangu ndio wenye ukomo kuna mahali wanafika hawawezi tena kuendelea mbele hata kama watataka kufanya hivyo,kwa sababu muda wa wao kunitumia umefika kikomo.
Kila kitu iinachofanyika chini ya jua kinapaswa kufanyika kwa kuzingatia muda. Muda uliotengwa kwa kila dhumuni ukitumika vizuri utayaona maisha yanakuwa mepesi.Ukifanya kila jambo kwa wakati nakuambia utafurahia mwenyewe maisha.Kinyume chake utanilaumu.
Kuna mambo usipoyafanya kwa kunizingatia mimi muda uwe na uhakika utahangaika kwa sababu kanuni ni kwamba kila jambo linafanywa kulingana na majira yake.Ukiwa mtoto yapo mambo ya kitoto kufanya na dunia haiwezi kukushangaa kwa sababu wewe ni mtoto.Ukiwa kijana yapo mambo unapaswa kufanya na ukiwa mtu mzima yapo mambo ambayo unapaswa kufanya. Kijana akifanya mambo ya kitoto dunia itamshangaa sana,na pengine mtu mzima akifanya mambo yanayopaswa kufanywa na vijana dunia itashangaa kwa sababu mtu mzima muda wa kufanya mambo kama kijana umepita na hautarudi tena.
Mimi naitwa muda naomba unipe thamani angalau kama ile mnayovipa vitu vingine mnavyoona vya thamani.Mnitumie vizuri maana kuwepo kwa ajili yenu ni swala la msimu haidumu milele. KIla jambo mfanye kwa wakati ili kuepuka matatizo siku za usoni.
Ukitaka kujipima ni namna gani unatumia muda mbona rahisi tu. Mambo unayofanya sasa yanalingana na muda ambao umeishi hapa duniani? Naitwa muda kazi yangu ni kutofautisha majira.Asubuhi ni muda,jioni ni muda,usiku na mchana ni muda,dakika,sekunde ni muda,siku ni muda,wiki ni muda,saa mwezi ni muda na mwaka ni muda.
Jamani nasema tena naitwa muda leo nimeamua kujitambulsiaha mwenyewe ili kujitoa kwenye lawama.Asiwepo mtu atakaeshindwa kufanya jambo kwa wakati halafu akanilaumu mimi eti alikuwa hajui. Nimejitoa kwenye lawama nisilaumiwe kwa lolote lile.Msinipoteze jamani mimi ni muhimu sana kwa maisha yako.Najua wengine wameachama hata kuendelea kunisikiliza wananishangaa leo ni mada gani hii ambayo ametuwekea? Nasema “NAITWA MUDA” sitaki uje kujuta labda uwe umechagua mwenyewe.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp:+255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com