Ulishinda Kabla Ya Kuzaliwa
Kila mtu anatamani kutambulika na jamii kuwa ni mshindi katika jambo lolote ambalo angeweka mkono maishani mwake.Lakini matokeo huwa kinyume, wanaoshinda ni wachache na idadi ya wanaosajiliwa upya katika daftari la wanaoshindwa inaongezeka kila siku.
Umewahi kujiuliza kwa nini mtu mwingine anashinda katika kila jambo analoweka mkono, huku mwingine akibaki kuwa kama mtazamaji kwa kushindwa kabisa katika mambo yote na kuongeza idadi ya watu wanaoshindwa katika mazingira yale yale ya maisha?
Ni muhimu kukumbuka kwamba kushinda au kushindwa kwa mtu,hakutegemei hali,uwezo,wala elimu aliyonayo tu; ili kuweza kushinda. Kushinda ni matokeo siyo tukio,ni namna mtu alivyo ndani mwake na anavyowaza moyoni mwake.Inapotokea udhihirisho ni picha tu ya mambo jinsi yalivyo ndani mwa mtu.
Ingawa wapo watu wenye elimu na uwezo wa fedha waliofanikiwa katika maisha,pia kuna watu wengi wa aina hiyo ambao wanaongoza kushindwa katika maeneo mbalimbali ya maisha yao.
Mhamasishaji mmoja wa nchini Marekani Merry Mossey anasema katika moja ya mafundisho yake kuwa kila kitu huumbwa mara mbili.Mara ya kwanza katika ulimwengu wa kufikirika (kiroho) na mara ya pili katika ulimwengu wa mwili. Cha kushangaza ni kwamba ulimwengu usioonekana ndio unaoendesha mambo katika ulimwengu halisi.
Mambo yote yanayoonekana ni nakala au matokeo ya matukio yaliyofanyika kabla katika ulimwengu wa kufikirika (roho) na kwa kweli ulimwengu wako usioonekana ndio unaoamrisha ulimwengu unaooneka.
Nataka kukumbusha mambo machache muhimu ambayo ukiamua kuyazingatia,yanaweza kukusaidia kupata taarifa muhimu kwa ajili ya kufanya uamuzi sahihi,kwa sababu watu wengi wamefanya maamuzi muhimu katika maisha bila kuwa na taarifa muhimu zinazohitajika kabla ya kuamua,matokeo yake kujikuta wanashindwa.
1.Kanuni ya mafanikio
2.Ulishinda kabla ya kuzaliwa
3.Huanza katika mtazamo (akili)
4.Matendo ni kila kitu
1. KANUNI YA MAFANIKIO
Kila kitu hapa duniani kinaongozwa na sheria na kanuni na mafanikio pia yanaongozwa na kanuni ambayo ukiifuata unakutana na matokeo chanya na ukiivuruga unakutana na matokeo hasi.Kanuni ni sheria na huwa haivunjwi,ikivunjwa basi anayevunja haimsaidii.Kwa kifupi japo kuwa haionekani kuwa tatizo,ukweli ni kwamba watu wengi wako gerezani baada ya kuvunja kanuni mbalimbali za maisha.
Ipo kanuni au sheria inayoongoza katika swala zima la mafanikio “the law of success “Sheria hiyo inasema hivi “
Kwa mfano kama unataka kumiliki fedha ya kutosha unahitaji kuwa na taarifa kwamba zipo kanuni zinazoongoza katika maswala ya fedha na waliofanikiwa ni wale wanaotunza kanuni hizo na kuzitumia katika shughuli zao,iwe biashara,huduma au kazi.
Kuna msemo wa kizungu unaosema “information is power” taarifa ni nguvu.Kabla mtu hujafanya maamuzi yoyote mazito hasa yanayoathiri maisha yako na watu wengine unahitaji kuwa na taarifa za kutosha kukuwezesha kufanya maamuzi bila kukosea sana.
Inawezekana kabisa wewe ni miongoni mwa watu wanaoamini kabisa kwamba taarifa ni nguvu na tunaishi katika zama za taarifa,lakini ni mara ngapi tumefanya maamuzi hata wakati mwingine maamuzi magumu bila kuwa na taarifa za kutosha na kujikuta maamuzi yetu yanatugharimu?
Watu wasiofanikiwa katika eneo la fedha ni wale ambao ama kwa kujua au kwa kutokujua wameshindwa katika shughuli zao kuzingatia kanuni na kujikuta hawafanyi vizuri katika maisha,kutokana na maamuzi waliyofanya bila kuwa na taarifa za kutosha kuwasaidia kuamua vizuri.
2.ULISHINDA KABLA YA KUZALIWA
Maisha ni fursa ambayo haipaswi kuwa na mipaka ya aina yoyote mtu kufikia kilele anachotaka kufikia,“Kila aliyezaliwa ni mshindi” Kuna ukweli unaothibitishwa na wana sayansi kwamba mtoto anapotungwa mimba ni matokeo ya mshindi mmoja miongoni mwa mamilioni ya mbegu zilizokuwa zinapambana kuwania ushindi wa nafasi moja ya kutunga mimba.
Watu wengi hata waliosoma vizuri elimu ya baiolojia hawakumbuki kama kabla ya mtoto kuzaliwa tayari huwa ni mshindi akingali katika tumbo la mama yake, Kama inavyothibitishwa kisayansi kwamba,wakati wa mimba kutungwa huwa kuna aina fulani ya ushindani mkubwa wa mayai kugombania nafasi ya kuwa kwenye tumbo la mama kwa ajili ya kuandaliwa kuzaliwa katika namna ya mwili.
Sisi sote tulitungwa mimba tukadumu ndani ya matumbo ya mama zetu kwa muda wa miezi 9 ndipo tukazaliwa,hivyo kumbuka kila mjamzito unayemwona amebeba mshindi au washindi ndani ya tumbo lake kwa wale wanaobeba mapacha.
Inasemekana kwamba mimba ya mtoto inapotungwa huwa kuna mayai milioni 300 yakishindania nafasi ya kutunga mimba na anapojitokeza mmoja kushinda,basi huwa mamilioni ya mbegu zimekosa fursa ya kushinda katika mchuano huo mkali.
Kwa kuwa mabadiliko yoyote unayotaka kufanya mtu ili yafanikiwe lazima yaanzie kwenye akili ndipo yadhihirike kwa vitendo katika mwili. Mfano huo wa ushindani wa mtoto kuwania nafasi ya kuwa mtoto ukusaidie kila utakapofika mahali ama kukata tamaa au kukatishwa tamaa na watu.
Kabla hujajitamkia na kukiri kushindwa kila binadamu anapaswa kutafakari kwa kina jinsi alivyoumbwa na Mungu na kwamba wewe ni mshindi kabla hata ya kuzaliwa hivyo ulizaliwa mshindi na kushindwa linaweza kuwa ni jambo la kuchagua kwa kuwa kila kitu kimeumbwa mara mbili.
Kama watu wote wangekuwa wanakumbuka ukweli huu unaothibitishwa na wanasayansi,basi dunia ingekuwa ni mahali ambapo kuna matokeo makubwa ya kazi za washindi ambazo zingedhihirika na kufuta kabisa msamiati dhaifu wa kushindwa katika chochote ambacho angeamua kufanya.
3. HUANZIA KATIKA MTAZAMO
Kushindwa au kushinda siyo jambo linalotokea kama ajali,ni matokeo ya uumbaji wa mtu katika akili yake ambao anaufanya kabla ya kudhihirisha kushindwa au kushinda katika ulimwengu huu wa mwili na nyama.
Kama mtu ndani yake anawaza katika jambo fulani kushinda na kuamini moyoni mwake kabisa kuwa anakwenda kushinda mtu huyo atashinda kwa sababu anayo sababu ya kushinda na imani inamsaidia kudhihirisha huo ushindi.Kinyume chake,kama mtu huyo moyoni mwake anaamini katika kushindwa,kwa nini ashinde? Lazima atashindwa kwa sababu tangu moyoni mwake ameamini na kuweka msingi wa kushindwa,hivyo anayo sababu ya kushindwa.
Sheria ya uvutano (Law of Attraction) inatukumbusha kuwa kile unachowaza mara kwa mara ndani mwako ndicho utakachovutia maishani mwako.Mawazo ni kama mbegu na unapoipanda uwe na uhakika mavuno hayatakwenda tofauti na ile mbegu uliyopanda.
Mtu anavyowaza moyoni mwake ndivyo atakavyokuwa.Ukipanda mafanikio akilini mwako utavuna mafanikio na ukipanda kushindwa basi utavuna kushindwa.Apandacho mtu ndicho atakachovuna.Huwezi kupanda machungwa halafu ukategemea kuvuna mapera itakuwa muujiza.
Watu wengi wanaposhindwa kufanya kitu hukimbilia kulaumu watu,wazazi labda kwa kutokuwasomesha vizuri,mazingira au hali ya uchache wa raslimali fedha kwa kuwa wanatoka labda familia maskini na kusahau kabisa mtuhumiwa namba moja kulaumiwa kuwa ni wao wenyewe.
Tunayo mifano mingi ya matajiri ambao wala hawakupata bahati ya kusoma vizuri lakini leo wanaheshimiwa hata na maprofesa kutokana na matokeo ya kuwepo kwao ni makubwa.Mfano hapa nchini ni tajiri Said Bakhresa hana elimu ya kutosha ya darasani laikini anaajiri watu walisoma katika miradi yake.
4.MATENDO NI KILA KITU
Ukishajua kuwa kama ilivyo kwa vitu vyote duniani huongozwa na kanuni,mafanikio pia yanaongozwa na kanuni,ukajua kuwa ulikuwa mshindi kabla hata ya kuzaliwa;tena ukakumbuka kuwa kila kitu huanza katika akili (mtazamo),baada ya yote hayo jambo la mwisho ambalo ningetaka ujue ni matendo.
Kuwa na taarifa bila kuchukua hatua kuweka yale unayoamini katika matendo na kufanya mara kwa mara,hakuna mabadiliko yoyote unayoweza kuleta katika maisha yako.Hakuna jambo rahisi kufanya kama kushindwa kwani kila siku mamilioni ya watu duniani wanahitimu na kuingia katika kundi la wanaoshindwa.
Idadi kubwa ya watu walioshindwa katika mambo mengi katika maisha ni wale wanaoongea sana bila kutekeleza chochote wanachoamini wangekifanya wangefanikiwa.Kuongea ni jambo moja na kutenda ni jambo lingine.
Ukifanya,ukafanya,ukafanya mara kwa mara hutafanikiwa tu,bali utaweza kubadilisha baadhi ya tabia na kujikuta unakuwa na tabia ya kufanya jambo fulani kama washindi na mwisho wa siku unakuwa ni miongoni mwa watu walifanikiwa wa kutiliwa mfano na watu wengine.
Kama umefuatilia vizuri makala hii unao uwezo ndani mwako kuwafanya kikawa kitu chochote utakachoamua kufanya na ukafanikiwa,iwe ni biashara,au kazi au katika huduma unayotoa kwa ajili ya kugusa maisha ya watu na kutimiza kusudi la kuwepo kwako hapa duniani;hakuna cha kukuzuia.
Hebu nikuachie zoezi fupi leo ninapohitimisha makala yangu:angalia katika jamii,mji,mkoa,nchi au sehemu kama kuna mtu yeyote unayemfahamu ambaye amefanikiwa.Ukishampata mtu wa namna hiyo anza kujifunza kutoka kwake namna anavyoishi na kuendesha mambo yake. Nini kinachomtofautisha na watu wengine?
Kuna kitu kikubwa utajifunza kutoka kwa mtu huyo na hapo basi unaweza kunakili na kufanya hivyo hivyo katika maisha yako;kumbuka ndege wanaofanana huruka pamoja.
Maisha ni fursa bila mipaka na hakuna kitu kinachoweza kukuzuia kufanya jambo lolote unalotaka kufanya madhari ukiamua na Mungu akiendelea kuturuzukak. Acha kujiwekea mipaka kwa kuwa unavyofikiri moyoni mwako ndivyo ulivyo pia.Kufanikiwa au kutokufanikiwa kwako hakutegemei elimu,hali au mazingira.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
WhatsApp: +255784503076
maishanifursa2017@gmail.com