JINSI YA KUJIONGEZA THAMANI
Watu wengi usiku na mchana wanahangaika kutafuta pesa kama njia ya kuwawezesha kumiliki zaidi wakiamini kwa kufanya hivyo wako katika njia sahihi ya kuyaelekea mafanikio. Huduma na kazi nyingi za wito zimeishia njiani baada ya watu kukosea mahali pa kuanzia kwa kutoa kwanza kipaumbele kwenye mafanikio ya pesa na kufanya wito kuwa kipaumbele cha pili matokeo yake wanapishana na pesa.
Kama unataka kufanikiwa katika maisha usihangaike kutafuta mafanikio au kutafuta pesa bali tafuta kuwa mtu wa thamani. Thamani ndicho kitu kitakachokufanya wewe mwenyewe kuwa na thamani na watu kuja kukuona na kujitofautisha na watu wengine.
Kwa mujibu wa hayati Dr Myles Munroe kama unataka kufanikiwa katika maisha usitafute mafanikio bali tafuta kuwa mtu wa thamani kwanza,kwa nini? Kwa sababu ukiwa mtu wa thamani kuna watu wengi hapa duniani ambao wanatamani kujiongeza thamani hivyo watakuja kwako kutafuta na kuchota thamani kutoka kwako na kwa kufanya hivyo watakuwa tayari kukulipa kwa hiari kwa kazi yako ya kuwaongezea thamani.
Karibu tena katika mtandao wetu ili tuweze kushirikiana pamoja kula chakula hiki cha akili, ambapo leo nataka kukushirikisha kipande hiki muhimu ambacho sehemu kubwa nimejifunza kutoka kwa hayati mch. Dr Myles Manroe.
Kama unataka kuwa mtu wa thamani unapaswa kuwa na taarifa juu ya mambo muhimu ya kuambatana nayo kujiongezea thamani, ili dhamira yako kugusa maisha ya watu wengine iweze kutimia. Ukiwa mtu wa thamani siyo tu watu watakushangaa bali watatamani kuja kujifunza kutoka kwako na kwa kufanya hivyo utakuwa na uwezo wa kuathiri maisha yao kwa kuwaongezea thamani pia.
Kimsingi hupaswi kuhangaika sana kutafuta mafanikio kupitia pesa badala yake fanya mambo ambayo yatasababisha watu kukutafuta wenyewe na kukuletea pesa kwa kuwa kuna kitu cha pekee wanakipata kutoka kwako kwa ajili ya maisha yao. Hali hiyo itakupa fursa pia ya kujinyima kwa hiari yako mwenyewe baadhi ya mambo ambayo unajua kwa kuyafanya yatasaidia kukupunguzia thamani badala ya kukuongezea hivyo utayaacha yapite hata kama moyo wakati mwingine unatamani kuyafanya.
Huwezi kuwa mtu wa kuongeza thamani kwa watu wengine, kama wewe siyo mwanafunzi kwanza anaetafuta kujiongeza thamani katika maisha yake kila siku. Mwalimu kila siku ni mwanafunzi na kwa kufanya hivyo anapata maarifa na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwasaidia wanafunzi wake vizuri zaidi.
Jambo moja kubwa ambalo unapaswa kuanza nalo kabla ya kuanza kutekeleza wito wowote linapaswa kuwa ni kujua au kuwa na MAONO. Maono ni kitu muhimu cha msaada sana katika maisha kwani husaidia kusudi la mtu katika maisha kutimia haraka,kwa sababu maono humsaidia mtu kuwa na picha ya kule anakotaka kufika kuanzia mwanzo na kukupa nidhamu ya kuchangua mambbo gani ushiriki na yapi uyapishe yapite hata kama yanaonekana kuwa mazuri kwani huwezi kushiriki katika kila tukio.
Katika kitabu cha mithali 29:18 kutokana umuhimu wa jambo hili la maono linasisitizwa kwa mkazo mkubwa. “Pasipo maono, watu huacha kujizuia;bali ana heri mtu yule aishikaye sheria” Ufunguo wa kwanza wa maisha ya mwanadamu ni maono katika maisha kwani maono ndicho chanzo cha nidhamu na mtu yeyote mwenye nidhamu ni rahisi sana kuvutia watu wengine kuja kujifunza kwake.
Nidhamu hujenga kujiamini mwenyewe na watu kukuamini pia kulingana na nidhamu fulani uliyojiwekea katika maisha na kama wewe utabaki katika mtazamo wako bila kuyumbishwa na kitu chochote. Nidhamu ni nguvu na kulingana na neno nidhamu ni tunda la maono.Kuna vitu utaviruhusu katika maisha yako na kuna mambo ambayo kwa namna yoyote ile hutayaruhusu yapate nafasi utayapisha yapite.
Watu wengi kwa kukosa maono wamejikuta wanaingia katika mtego wa kufanya karibu kila kitu kinachokuja mbele yake anachokutana nacho na kufukuzia kila fursa, matokeo yake wanajikuta wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea wenyewe kwa sababu wanataka kufanya kila kitu.
Kama unajua unakoelekea ni rahisi kuanza safari na kwenda moja kwa moja unakotaka kufika kwa sababu pia unaijua njia itakayokufikisha huko kwa urhisi. Kama unajua unakoelekea hutabadili mwelekeo kwa kuwa njia na kitu sahihi unachoendea unakijua.
Umaskini siyo tatizo isipokuwa ni matokeo.Watu wengi wanakuwa maskini kwa kuwa hakuna mtu anayejua wao ni nani. Maono humtambulisha mtu mbele ya watu. Wakati watu wanapofikiria juu ya swala fulani hawataacha kukufikiria wewe kwa sababu wewe ni mtu wa thamani.
Ufanye nini ili kujiongezea thamani?
Hakuna binadamu aliyetimia katika kila eneo wala anaeweza kufanya kila kitu.Kuna mambo machache hapa ya kuzingatia ili kujiongezea thamani na kuwa mtu wa kuongezea watu wengine thamani.
Tambua kusudi la kuwepo kwako
Mwenyezi Mungu alipokuumba na kukupa fursa ya kuishi katika dunia hii alikupa pia na wajibu maalum kwa ajili ya kuihudumia dunia.Yamkini wito wako haufanani na mtu mwingine yeyote.
Kwa nini Mungu aliamua wewe uwe wewe? Kwa nini hukuwa kitu kingine tofauti na kwa nini unaishi? Majibu ya maswali hayo yatakupelekea kutambua kusudi la kuwepo kwako na kuanza kuliishi.
2. Tafuta maarifa kutoka kwa watu wengine
Ni muhimu sana kutafuta maarifa kupitia njia ya kujifunza kutoka kwa watu wengine ili uweze.Soma vitabu,hudhuria semina na makongamano ya watu wengine wanaofundisha kitu unachoona kitakusaidia kukuvushwa kutoka hatua moja kuelekea kuanza kuliishi kusudi la kuwepo kwako duniani.
3. Fanya mazoezi
Haitoshi kujifunza halafu ukakaa tu ni lazima uweke kwenye vitendo kile kilicho ndani mwako.Anza kufanya mazoezi kuelekea kule unakotaka kufika na utaona thamani yako inapanda kadri unavyoendelea.
Achilia kile unachoamini umebeba ndani mwako wala usikubali mtu kukupima kwa kile ambacho hakijui kwani aliyebeba maono ni wewe. Hakuna aliyefanikiwa kwa kuwaza tu lazima kuweka kwenye matendo maono yako.
Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au WhatsApp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu +255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com