Tofauti Ya Kazi Na Wito

Umewahi kujiuliza kuna tofauti gani kati ya wito na kazi? Ingawa watu wengi wanachanganya maana ya maneno haya mawili muhimu katika maisha na kujikuta wanazungumzia wito mahali pa kazi na kuzungumzia kazi mahali pa wito,ipo tofauti kubwa kati ya kazi na wito.

Mahangaiko hayo ya kutofautisha wito na kazi ni matokeo ya watu wengi kutokujua hasa kusudi la kuwepo kwao hapa duniani. Ni muhimu kukumbuka kuwa kila mtu aliyepata nafasi ya kuumbwa na Mungu na kuishi hapa duniani ni kwa sababu na kusudi maalum.

Kazi ni shughuli yoyote halali ambayo mtu anafanya ili kujipatia mahitaji ya kila siku kwa ajili yake na wale wanomtegemea. Shughuli halali kwa sababu zipo kazi zingine haramu ambazo hatuwezi kuzipa sifa ya kazi. Wito ni lile kusudi la kuumbwa kwako.Kile kitu Mungu alichokuitia kufanya hapa duniani ndio wito.

Karibu tena katika makala zetu za kujenga katika mtandao wetu. Kwanza nikushukuru sana kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu. Kazi hii ina maana tu kwa sababu wewe upo. Kama ni mara yako ya kwanza kusoma makala zetu nikukaribishe kwa mikono miwili na kuahidi kuwa hutakaa ujute kuufahamu mtandao huu.

Iko tofauti kubwa sana ya kuhudumiwa na mtu anayefanya anachofanya kama wito ndani mwake mtu anayefanya anachofanya kama kazi na hawatakaribiana kwa namna yoyote katika utendaji wao wa kila siku.Kimsingi kinachokosekana leo ni watu wenye wito katika maneo mbalimbali na hali hii inashusha sana tija katika huduma.

Watu wengi wanashindwa kutoa huduma kwa ufanisi kwa kushindwa tu kutofautisha kati ya wito na kazi na matokeo yake wameshindwa kutoa mchango ambao wangestahili kutoa hapa duniani.Kufanya jambo lolote bila wito ni kama mzigo.Bila shaka waweza kuwa miongoni mwa watu wale ambao wanatamani kufanya kazi kwa kuzingatia kusudi la kuitwa kwao hapa duniani.

Kila kazi unayoifanya unapaswa kuzingatia wito wako ili uweze kutoa huduma kwa ufanisi. kazi ni ibada ambayo ukiifanya kwa uaminifu ukizingatia maongozi ya Mungu utampendezesha na kusababisha ufalme wake kushuka hata kwenye kazi au huduma unayotoa.Haijalishi wewe ni mchingaji,mwalimu,mfanya biashara au vyoyote unavyoweza kutaja, wewe ni mtumishi uliyeletwa kwa kusidi maalum.

Ngoja nikushirikishe njia rahisi itakazokusaidia kutambua kama unachofanya ni wito au ni kazi ili uweze kujisaidia wewe mwenyewe na kusaidia watu wengine kuondoka katika mahangaiko haya ya kutoa huduma bila kujua kama wanatimiza wito wao au lah.

UTAJUAJE KAMA UNACHOFANYA NI KAZI AU WITO?

Unaweza kuwa wewe ni mzuri sana katika eneo fulani unalofanya na kila unayemhudumia anaridhika kuwa umemtendea kwa kiwango cha juu lakini wewe moyoni mwako husukumwi kama umefanya kitu kinachogusa moyo wako,basi ujue hapo bado hujagusa eneo lililo ndani ya wito wako. Watu wanakiri kabisa kwamba wewe ni mzuri katika eneo husika lakini wewe moyoni huoni ukiri basi bado hapo unatumikia kazi siyo wito.

Watu wengi wanafanya kazi si kwa sababu wanazipenda kazi wanazofanya bali ni kwa sababu zinawasaidia kupata mahitaji yao ya kila siku na familia zao na hofu kubwa ni kwamba wanaogopa bila kufanya kazi hizo maisha yao yatakuwa magumu sana kwa sababu hawana njia nyingine ya kufanya kuendesha maisha.

Katika nyakati za leo tunao wataalamu wengi ambao walikwenda kusomea shahada za taaluma walizo nazo si kama wito kwao ila kwa sababu eneo hilo ndilo liliolokuwa na nafasi na uhakika wa kupata ajira wakimaliza masomo yao. Wako kazini wanalipwa mshahara kila mwezi kwa kazi ambayo siyo wito wao. Ni shida!!!!!

Wito ni pale hamu na shauku yako inapokutana na mahitaji ya jamii au dunia.Ni huduma au kazi unayofanya kwa moyo mweupe bila kujali kama unalipwa au hulipwi kwani malipo ya kwanza ya mtu mwenye wito ni kuwaridhisha kwanza watu anaowaowahudumia. Mtu mwenye wito lazima anufaishe watu engine bila kutilia maanani manufaa yake binafsi kwanza. Kwa maana hiyo kama mtu anafanya kazi ambayo inamnufaisha yeye peke yake pengine na familia yake tu;huo sio wito.

Jamb hili ndilo linalosababisha mtu asomee kitu fulani na baadaye kubadilisha kwa kusomea kile kitu anachosikia moyoni mwake bila kujali kama kazi anayoacha inampatia kipato au lah! Hujawahi kuona mtu anaacha kazi yenye mshahara mzuri halafu anakwenda kufanya kazi ya mshahara mdogo lakini anaridhika kabisa?

TAMBUA KAMA WITO WAKO NI KUTOKA KWA MUNGU AU LAH!

Upo wito kutoka kwa Mungu na upo wito tu ambao hautoki kwa Mungu.Katika zama hizi si rahisi sana kutofautisha mtu anayefanya kazi kama wito na asiyekuwa na wito kwa maneno tu ispokuwa kwa matendo na matunda ya kazi zao. Ili kujua kama wito wako ni kutoka kwa Mungu basi usiache kujiuliza swali hili muhimu:-

Kitu gani ninachopenda sana kufanya?

Mungu ameweka shauku kubwa ndani mwako mtu ili kumwezesha kutimiza wito alioitiwa kufanya hapa duniani. 1Kor. 9:16 “Maana,ijapokuwa naihubiri injili,sina la kujisifu;maana nimewekewa sharti,tena ole wangu nisipoihubiri injili”

Kazi au huduma unayofanya ambayo hainufaishi watu wengine huo sio wito. Wito kutoka kwa Mungu lazima mtu ndani mwake awe na msukumo ambao unamfanya afikirie kuhudumia watu kwanza bila kufikiri kama kuna namna yoyote atanufaika au la kwa sababu kila anachofanya ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu tu.

Malipo makubwa kwa mtu mwenye wito ni kushughulika na matatizo ya watu kwa kuyapatia suluhu na mtu wa namna hii utapima mafanikio yake kwa kigezo cha idadi ya watu watakakuwa wameguswa na huduma yake siyo pesa na akifanya hivyo basi pesa zitamfuata.

Kichocheo cha unachofanya kitakuwa ni kipimo muhimu cha kukujulisha kama unachofanya ni wito kutoka kwa Mungu au lah! Kama msukumo wako ni mafanikio ya kifedha kwanza badala ya mafanikio ya kiroho basi hiyo ni kazi siyo wito ni kazi kama kazi zingine na mafanikio yake hayawezi kugusa watu wengine.

Hiyo ndio tofauti kati ya mtu anayefanya kazi na yule anayehudumia mahali kama wito. Kinachopatikana kwa nadra leo katika mazingira ya kazi nchini kwetu na kwingineneko duniani ni watu wenye wito wanaojua wajibu na kusudi la kuwepo kwao hapa duniani.

Watu wengi wanaanza kufikiri kupata faida wao kwanza badala ya kujikita kutoa huduma kwanza bila kufikiri jinsi watakavyonufaika wao binafsi na matokeo yake wanapishana na mafanikio ikiwemo pesa. Tengeneza huduma, tatua matatizo ya watu,hudumia watu kwa moyo wote kana kwamba hutapata nafasi tena ya kuhudumia utaona mwenyewe jinsi ambavyo mafanikio yataanza kukutafuta. Kwa nini? Kwa sababu unacho kitu cha pekee.

Kama unataka kushinda katika kila jambo utakalofanya hapa duniani basi jitahidi sana kujua waito ulio ndani mwako ambao Mungu amekupa ili uweze kutoa huduma bila kuangalia kama kuna mtu mwingine anaeweza kutoa huduma kama yako kwa sababu huenda ikawa kilichomo ndani mwako kimebebewa na wewe tu katika eneo,wilaya,mkoa au nchi unaoishi.

Naamini kuna kitu cha kukusaidia utakuwa umepata kwenye makala hii fupi. Kama ungependa kuwasiliana kwa ushauri au ungependa kuingia zaidi kwa undani kwenye mada hizi,basi usisite kuwasiliana nami kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno,whatsap au kupiga simu.

Ni mimi mtumishi wako na kocha-Philipo Lulale
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com

WhatsApp+255784503076

Next
Next

Badili Uchungu Kuwa Wito