Anza Na Tabia Kubadilika
ANZA NA TABIA KUADILIKA
JINSI YA KUBADILI TABIA
“Natamani kubadilika na kuboresha maisha yangu katika eneo fulani,lakini nafika mahali nashindwa naendelea kufanya kitu ambacho sikipendi inaniumiza sana” Hebu fikiri unakutana na mtu anakushirikisha shida yake kwa maneno uliyotangulia kusoma hapo juu utamsaidiaje?
Mara nyingi nimekuwa nikiulizwa na watu swali hilo nami ushauri wangu umekuwa ukiwaacha wengi wakishindwa kuamini kwanza kile ninachosema ninapowajibu kwa urahisi tu “anza na tabia”. Ndiyo nasema anza na tabia kwa sababu ukianzia mahali vibaya utajikuta inakuchukua muda mrefu kuleta matokeo unayoyatarajia.
Sisi sote tuna eneo ambalo tungehitaji kufanyia mabadiliko au tumewahi kufanyia mabadiliko kwa ajili ya kuboresha maisha yetu na kugusa maisha ya watu wanaotuzunguka siku hata siku.Lakini imetuchukua muda mwingi Zaidi na pengine kufikia mahali tukashindwa kabisa kuboresha eneo hilo.
Ninachotaka kukushirikisha leo ni mbinu na maarifa kidogo yatakayokusaidia kuboresha maeneo fulani katika maisha yako ili uweze kufanya vizuri zaidi.Kwanza nataka nikuhakikishie unayo haki na uwezo wa kufanya zaidi ya unavyofanya sasa.
Inaweza kuwa ni wewe mwenyewe,au unataka kumsaidia mumeo,mke wako,rafiki yako,mwanafunzi mwenzako,mtoto wako ambaye anatamani kubadilka katika eneo fulani ni muhimu sana kujua pa kuanzia.Watu wengi wana taarifa kuwa wana matatizo katika maeneo fulani lakini wanashindwa kuboresha maoneo hayo kwa sababu tu hawajui waanzie na kumalizia wapi.
HATUA MUHIMU ZA KUPITIA
1.KWANZA FAHAMU ENEO
Ni muhimu sana kujua bayana eneo katika maisha yako ambalo ungependa kufanyia mabadiliko.Hatua ya kutambua eneo unalotaka kuboresha, ni hatua muhimu ya kukiri mwenyewe kwamba hufanyi vizuri katika eneo fulani na ungependa kufanya vizuri Zaidi ya unavyofanya kwa kuwa, unao uwezo ndani mwako usiozuilika. Bila kuwa na uhakika wa eneo ambalo una udhaifu ambao ungependa kuboresha itakuchukua muda mrefu kuboresha eneo lenyewe.
Kuna msemo unaosemwa sana na watu wengi kwamba,ile tu kujua tatizo tayari umelitatua tatizo hilo kwa sehemu kubwa.Kwa kifupi huwezi kutatua tatizo kama hulijui na mtu wa kwanza kujua tatizo lako ni wewe mwenyewe.
Kama unataka kujisaidia wewe mwenyewe kubadilika au unataka kumsaidia mtu aondokane na tatizo fulani, basi mahali pa kuanzia ni kuchunguza tatizo na mara nyingi utakuta chanzo ni tabia fulani aliyoanza kuijenga pole pole kwa muda mrefu na sasa imekuwa sehemu ya maisha yake ambayo ni ngumu kuivunja.
Inaweza kuwa ni tabia aliyojengewa kipindi chote alipokuwa katika hatua ya malezi ya wazazi au ni tabia ambayo alijiundia mwenyewe kulingana na msukumo wa jamii inayomzunguka.
2. TENGENEZA SABABU
Hatua nyingine katika kuelekea kufanya mabadiliko katika eneo fulani la maisha yako ni kutengeneza sababu ya wewe kufanya mabadiliko katika eneo husika.Sababu hii lazima izae maumivu, kwa hiyo fikiria hasara ambayo unapata kila siku,kila wiki,kila mwezi au kila mwaka kutokana na tabia hiyo.Fikiria kama hungekuwa katika hali hiyo ni hatua gani ungekuwa umepiga katika maisha yako na ungegusa watu wangapi katika hilo eneo.
Kumbuka unachopitia wako watu wengi wanakipitia na hawana namna ya kufanya kutoka.Ukifaulu utakuwa bingwa wa kujisaidia na kusaidia watu wengine kutatua changamoto zao.”master solutions”
Hebu fikiri umeishi duniani miaka kadhaa lakini ukijilinganisha na watu wa umri wako wamekuacha mbali katika maeneo mengi tu. Maumivu unayohisi moyoni mwako kwa kutokufanya kama wengine walivyofanya inaweza kuwa ni sababu ya kukuchoche kufanya mabadiliko tena kwa kasi ambayo hungeweza kama ungekuwa huna sababu nyuma yako inayokusukuma.
Hii ni muhimu sana itakusaidia kuwa na hasira ukikumbuka muda uliopoteza ukihangaika kwa kujua au bila kujua kama unahitaji kubadilika.Bila kuwepo sababu ya maumivu ni rahisi sana kuamua na kurudia katika hali yako ya kawaida;lakini ukikumbuka una maumivu tayari ndani mwako yaliyosababishwa na hali ambayo umekuwa ukiiona ni kawaida tu,ile hasira haitakuruhusu kurudi nyuma.
3.TENGENEZA MPANGO KAZI
Ukishabaini eneo ambalo ungependa kufanya mabadiliko,na kutengeneza sababu ya mabadiliko hatua ya tatu unapaswa kutengeneza mpango wa mabadiliko. Bila kuwa na mpango ni rahisi sana kuanza na kuishia njiani kabla hata hujaona matokeo unayotarajia.
Hatua ya kutengeneza mpango ni namna ya kutafsiri mawazo yako ya mabadiliko kutoka kichwani hadi kuyaandika kwenye karatasi.Hatua hii ni muhimu kwani ndiyo inayokuwezesha kuona mwisho wa jambo unalotaka kulifanya tangu mwanzo.
Mpango utakuonyesha hatua utakazopitia,gharama utakazolipa ikiwaili kuleta mabadiliko unayoyatarajia ikiwa ni pamoja na rasilimali fedha na muda utakaohitaji kwa ajili ya kufikia lengo.
4. KUFUMBA NA KUFUMBUA
Ingawa watu wengi hufikiri ili kufanya mabadiliko ndani ya mtu,anahitaji siku au miezi kadhaa kuweza kubadilika,ukweli ni kwamba kubadilika ni kitendo cha mara moja tu kwani mabadiliko huanzia ndani ya mtu kwanza.Watu wengi huchanganya mchakato na mabadiliko.Mhamasishaji mahiri wa nchini Marekani Anthony Robbin katika moja ya kitabu chake anasema “kubadilika ni kitendo cha mara moja”.Yaani ni kama kufumba na kufumbua macho unabadilika.
Kwa nini iko hivyo? Iko hivyo kwa sababu ili ubadili tabia fulani unaanza kwanza na mtu wa ndani ambaye akisha elewa anafanya maamuzi ya kubadilika mara moja. Mtu wa ndani akishafanya uamuzi wa kubadilika basi,kufumba na kufumbua unabadilika na kuanza kufanya matendo yatakayokusaidia sasa kutimiza azma ya mtu wa ndani aliyoyafanya. Kumbuka ulimwengu wa kufikirika ndiyo unaoendesha mambo yote yanayofanywa na mtu katika ulimwengu halisi.
Tabia unayotaka kubadilisha ni mtu wa ndani huyo huyo alifanya uamuzi wakati fulani kwa kujua au bila kujua na akaanza kidogo kidogo kufanya mazoezi na mwisho wa siku ikawa sasa ni tabia yako.Wataalam wa saikolojia wanabainisha kuwa mtu akifanya kitu mfululizo kwa wiki tatu basi inabadilika kuwa tabia.Na ikisha kuwa tabia basi inakuwa sehemu ya maisha yake anaishi nayo.
Chanzo cha mtu wa ndani kufanya mabadiliko ni ile sababu iliyozaa maumivu na sasa kujielekeza tu kwenye kufanya mabadiliko,uvumilivu tena kusubiri unaisha.Kwa kuwa mtu wa ndani hana mzaha katika eneo hilo tena anataka kubadilika nafsi tayari ina picha ya namna hali itakavyo kuwa mabadiliko yakitokea.Kwa kifupi anayo picha ya ndani ya mwisho utakavyokuwa baada yakufanya mabadiliko.
Kwa mfano una tatizo la kuchelewa kurudi nyumbani iwe kwa sababu ya msingi au isiyo ya msingi.Kwanza kabisa fahamu kuwa tatizo sio wewe kufika nyumbani kwa kuchelewa ila ni mazoea ya kuchelewa uliyojijengea ambayo imepelekea kuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani. Jiulize kwa nini sasa una tabia ya kuchelewa nyumbani? Ni hasara zipi unapata kwa kuchelewa kurudi nyumbani?.
Yaweza kuwa una watoto wadogo ambao kwa sababu ya tabia yako ya kuchelewa wanakosa kuwa na wewe karibu.Ili uwe na sababu yenye nguvu na maumivu katika kesi hii jiulize,hivi ni kweli watoto wako sio muhimu kuliko sababu inayokufanya uchelewe? Hebu nielewe kidogo kila siku baada ya kazi unajumuika na wenzako kwenda bar kunywa mpaka usiku wa manane ukirudi watoto wako wamelala na siku za mwisho wa wiki hushindi nyumbani.
Kwa tafsiri rahisi ni kwamba kwako umeyapa thamani mambo yasiyo ya msingi na kusahau yaliyo ya msingi. Kumbuka mzazi ni kocha kwa watoto wake kuna mambo mengi wanapaswa kujifunza kutoka kwako kwa kauli na vitendo pia. Huo ni mfano tu kesi moja inaweza kuwa tofauti na hiyo.
Ukishafanya uamuzi ndani mwako wa kufanya mabadiliko basi mchakato unakutaka uanze utekelezaji kidogokidogo.Mfano una mazoea ya kuchelea kurudi nyumbani kila siku jioni unarudi watoto wamelala na sasa unafika mahali pa kuanza kuichukia hiyo hali,usijaribu kuanza kuacha kwa ghafla hutafika mahali.
Kama ulikuwa unakaa vikao vinne kwa siku kabla ya kuelekea nyumbani,sasa punguza hivyo vikaao.Kidogo kidogo utajikikuta unaanza kuacha na mwisho wa siku unafaulu kuondokana na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani.
Kwa nini tunapaswa kuanza kidogo kidogo kufanya mabadiliko na kuja kuwa tabia yako? Kumbuka tabia unayojaribu kupingana nayo haikujengwa siku moja ila ilijengwa kwa muda mrefu kidogo kidogo na mwisho kuwa tabia hivyo huwezi kuiondoa mara moja. Nimalize tu kwa kusisitiza kuwa kama unataka kubadilika katika eneo lolote basi anza na tabia. Chukua hatua.
Naamini kuna kitu utakuwa umejifunza kwenye Makala hii fupi. Kwa ushauri au kuingia ndani Zaidi ya mada hizi usisite kuwasiliana nasi kwa kutumia njia za mawasiliano hapo chini,njia ya ujumbe mfupi wa simu,whatsap au kutembelea endelea kufuatilia Makala zetu.
Ni mimi mtumishi wako na kocha Philipo Lulale-
WhatsApp +255784503076
maishanifursa2017@gmail.com