Muda Na Mabadiliko
Hakuna Kinachoweza Kuzuia Mabadiliko
Tangu tusherehekee January 1 kuupokea mwaka 2024 wala si muda mrefu sana.Ilianza siku,ikatengeneza wiki,nayo wiki ikatengeneza mwezi na mwisho miezi ikatengeneza jumla ya miezi 12 ambayo kwa pamoja imepewa jina la mwaka 2024.
Kinachoniumiza mwenzenu siyo mwaka kwisha kwa sababu 2024 siyo mwaka wa kwanza kwisha,kuna miaka mingi imekuja na kupita;ila kila ninapotafakari kuwa sitakaa nikuone tena mwaka 2024 pamoja na miezi yako mpaka nitakapomaliza safari yangu katika dunia hii inanitisha.
Karibu tena katika makala zetu za kujenga kwenye mtandao wetu. Kwanza nikushukru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu. Kazi hii ina maana kwa kuwa upo wewe unaefuatialia kivyume chake haina maana.
Tulivyokuwa tunaishi tulidhani kwamba wewe ni mwenzetu na kwa kuwa tulikuzoea sana tukajisahau hatukufikiri kama hungekaa ukatuacha kama wakubwa zako kina 2021,2022, 2023 na kadhalika walivyotuacha.
Watu wengi kila inapofika kipindi cha mwisho wa mwaka hujikuta katika hali kana kwamba mwaka umekwisha kwa ghafla wakiwa bado hawajajiandaa. Ukiangalia mambo uliyokuwa umepanga kufanya na yale uliyofanikiwa kuyatekeleza unakuta kwamba malengo mengi hujayafikia.
Utangulizi huo nataka utusaidie kutafakari juu ya vitu viwili muhimu katika maisha ya binadamu yeyote nikiwemo mimi na wewe yaani MUDA na MABADILIKO. Hayati mchungaji Dr Myles Munroe anaeleza kuwa nguvu mbili kubwa katika dunia hii ni muda na mabadiliko.
Muda na mabadiliko ni kitu cha lazima katika maisha ambacho kila mtu lazima ashughulike nacho awe ana taka au asitake chenyewe kipo tu. Mabadiliko yatatokea ukishiriki kuyaleta au hata usiposhiriki kuyaleta yenyewe yatatokea tu.
Muda utasogea pamoja na wewe au hata bila wewe hautakusubiri hata siku moja uwe unajua au hujui.Hakuna kitu kimoja katika maisha kinachoweza kuzuia vitu hivi viwili kutokea mabadiliko na muda.
Ukitaka kufanikiwa lazima ujifunze namna ya kuongoza muda na mabadiliko. Ufunguo wa mafanikio ya ufalme hapa chini ya jua ni kuwa na maarifa yatakayokusaidia kuwa mwanzilishi na mpanga mabadiliko.
Watu wote jinsi tulivyo kila asubuhi tumepewa bila upendeleo wa aina yoyote vitu hivi viwili muda na mabadiliko.Hakuna aliyezidishiwa muda au aliyepungukiwa muda.Vile vile hakuna aliye tajiri wa mabadiliko wala masikini wa mabadiliko.Mabadiliko hutokea kwa mtu yeyote mahali popote.
Siri kubwa ya mafanikio hapa chini ni kufanikiwa katika kupanga kusimamia muda na mabadiliko. Unaweza kuwa na ndoto kubwa ya kufanya mabadiliko makubwa;hiyo itabaki kuwa ndoto tu mpaka pale utakapokuwa umeanza kuitafsiri hiyo ndoto kwa namna ya mpango.
Mabaadiliko yanatokea katika nchi ya Tanzania kama yanavyotokea huko Amerika,mabadiliko ya watu na vitu ni jambo la dhahiri. Mimi na wewe tunapita katika hatua muhimu za mabadiliko ya kimaumbile.Wakati tukingali tumboni mwa mama tunakuwa wachanga kabisa wala hatujui kinachoendelea. Muda wa mabadiliko unapofika tunajikuta tunazaliwa na kuongeza idadi ya wakazi hapa duniani.
Tunakuwa watoto wadogo na mabadiliko yanatusukuma kukimbia utoto na kuwa vijana. Ujana unakimbizwa na mabadiliko na kujikuta tunageuka sasa kuwa watu wazima na mwihso wa siku tunaingia katika uzee. Muda na mabadiliko siyo kitu cha kushindana nacho bali kuifunza jinsi ya kuenenda nacho.
Tukizingatia kwamba hatuna mji unaodumu hapa duniani na muda wangu mimi na wewe ni mfupi sana kuishi hapa duniani,ni jambo la msingi sana kutilia maanani hatua ya kupanga namna ambavyo tutatumia muda wetu hapa duniani.
Kama mwaka 2018 hukufanikiwa kuishi kulingana na jinsi ulivyokuwa umepanga,au hukuwa na mpango kabisa na matokeo yake kujikuta umeishi chini ya kiwango ulichokusudia wewe mwenyewe,ni wakati muafaka sasa kukaa chini kutafakari na kuanza kupanga namna utakavyokwenda kutumia muda wako mwakani,
Sisi sote tumepewa karama mbalimbali kupanga ni kitendo cha kuratibu muda ulio nao kati ya kuzaliwa na kufa. Kuna mambo mengi sana yanayotafuta kutumia muda wako kwa kujua hata bila kujua.
Kama hutaweza kujipangia namna ya kudhibiti na kusimamia muda wako mwenyewe uwe na uhakika kwamba wengine wanakupangia namna ya kudhibiti muda wako na namna ya kuutumia kwa manufaa yao.
Ni wakati muafaka tunapomaliza mwaka ujitafakari na kuanza kuandika mpango kazi wako wa miaka inayokuja mbele yako ili uweze kuanza kushi kwa matumaini ya kufanikiwa. Bila kupanga namna ya kutumia muda na kukabili mabadiliko,yatakuja na kukuacha hayatakusubiri.
Usihofu kutafuta ushauri kwa watu wengine wanaoweza kukuongoza kuweza kutimiza azma yako ya kuwa na mpango wa shughuli zako. Katika kitabu cha Mithali 20:18 Biblia inasema “kila kusudi hudhihirika kwa kushauriana, na kwa shauri la akili fanya vita”
Kuwa na uwezo wa kupanga maisha yako ndicho kitu pekee kitakachokutofautisha na wanyama wengine. Kupanga ni kumaliza kabla ya kuanza. Kuiona safari kabla hata hujaianza.
Hebu chukua muda mfupi uanze kufunua hadithi ya kitabu chako cha maisha ulichoandika mwaka 2018. Ni mambo mangapi yametokea bila wewe kuwa na taarifa na mangapi yametokea ukiwa na taarifa?
Hujachelewa wakati wowote unapogundua kuwa unahitaji kupanga muda na kudhibiti mabadiliko usisite kuanza kupanga maisha yako. Haijalishi una miaka 60 au 16 wewe anza kupanga utaona kila kitu ulichokuw aunatamani kufanya miaka mingi bila mafanikio kinatimia. \
Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu +255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com