Pesa Siyo Msingi Pekee wa Mafanikio

Picha kwa hisani ya mtandao

Kuna kitu kimoja kinachonishangaza kila mara—watu wanapata pesa, lakini wanazichezea. Ni kama hawaoni fursa zilizo mbele yao. Badala ya kuzitumia kubadilisha maisha yao na ya familia zao, wanazitelekeza kama maji yaliyomwagika chini.

Lakini je, pesa pekee yake ndiyo msingi wa mafanikio?

Mtu mmoja aliwahi kujiambia, "Nikipata pesa nzuri, sitayapoteza maisha yangu bure. Nitajenga nyumba yangu, nitawekeza, nitanunua hisa kwenye makampuni ili fedha hiyo inizalishie zaidi na kuleta uhakika wa kesho yangu." Haya ni mawazo mazuri, lakini uhalisia mara nyingi huwa tofauti kabisa na mipango yetu hasa pale pesa inapoangukia mikononi mwetu.

KISA CHA TUPATUPA

Tupatupa alikuwa msanii wa uchongaji wa vinyago. Kipaji chake kilikuwa cha kipekee, lakini kwa muda mrefu, alihisi kama dunia haimtambui. Aliendelea kufanya kazi kwa bidii, huku akimuomba Mungu amfungulie milango ya mafanikio. Siku moja, wageni kutoka nje ya nchi waliona kinyago chake kikiwa na saini yake. Wakavutiwa, wakaanza kumtafuta, na hatimaye, wakampata na walimpeleka nchini Ufaransa kuonyesha ujuzi wake. Ndoto yake ilikuwa imetimia—kipato chake kiliongezeka mara dufu!

Baada ya mwaka mmoja, aliamua kurudi nyumbani akiwa na pesa nyingi. Ndugu, jamaa, na marafiki walimlaki kwa shangwe. Wote waliona kuwa sasa Tupatupa alikuwa mtu wa mafanikio. Kutoka uwanja wa ndege Tupatupa alikodisha magari matatu: moja kwa ajili ya kumbeba yeye, moja kwa ajili ya kubebba begi zake tatu za fedha na mlinzi na moja kwa ajili ya kubeba ndugu zake wachache waliokuja kumpokea.

Lakini Tupatupa hakuwa na mpango madhubuti wa fedha kwani alianza kutumia pesa zake kwa anasa, sherehe, na kusaidia kila mtu aliyemzunguka bila mipaka ili mradi tu amekuja kwake akiwa analia shida. Wapambe wakamzingira—walimwimbia nyimbo za sifa, walimbebea hata koti lake! Kila kona aliyoenda, alikuwa mfalme wa mtaa.

Aliamini kuwa ana muda wa kutosha kujenga nyumba, kuwekeza, na kufanya mambo makubwa. "Fedha ipo," alijisemea.

Lakini ndani ya miezi minane tu, fedha zilianza kupungua. Wale waliokuwa karibu naye walianza kupotea, sherehe ziliisha, na alipochungulia mabegi yake, pesa ilikuwa imeyeyuka.

Ndoto alizokuwa nazo kabla ya kupata pesa zilianza kumrudia—lakini sasa hakuwa na chochote cha kuzitekeleza. Alilazimika kurudi kule alikoanzia, akakaa chini tena na kuchonga vinyago, safari hii akiwa na somo kubwa maishani mwake:

Mali bila daftari hupotea bila habari.

SOMO KUTOKANA NA KISA CHA TUPATUPA

Sasa ni zamu yako.

  • Je, unajifunza nini kutokana na hadithi ya Tupatupa?

  • Ni kiasi gani cha pesa kimepita mikononi mwako, lakini bado hujaweza kutimiza ndoto na malengo yako?

  • Je, unahisi hadithi hii inagusa maisha yako kwa namna gani?

Mafanikio siyo pesa tu—ni nidhamu ya pesa, ni mipango thabiti, na ni kuelewa kuwa kila shilingi unayoipata ni fursa ya kujenga kesho yako.
Naamini utakuwa umepata kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Kama kuna namna unafika mahali hujui mahali pa kuanzia ili uweze kupata kutambua kusudi la kuwepo hapa duniani basi tunakukaribisha tuwasiliane tutakusaidia. Bofya mahali palipoandikwa “USHAURI NA MAFUNZO BOFYA HAPA” nasi tutakufikia mapema.
Ningependa kusikia maoni yako! Unaweza kuwasiliana nami kwa WhatsApp, ujumbe mfupi wa maneno, au simu kwa namba yangu hapa chini.

Ni mimi, rafiki na kocha wako,
Philipo Lulale
WhatsApp: +255 784 503 076
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Alianza Kinyonge Akamaliza kwa Ushindi!

Next
Next

Anza Na Tabia Kubadilika