Hakuna Jambo Lisilowezekana

Inawezekana Ukiamini

Unakumbuka moja ya makala zangu ambayo nimewahi kuandika kwenye mtandao huu inayoitwa “kuna fursa katika kila hali? Ukiunganisha na dhana ya maisha ni fursa ambayo haina mipaka na hiki ninachokwenda kukushirikisha leo utakubaliana nami kabisa kuwa kila hali imeficha fursa. 

Karibu tena msomaji wa makala zetu kwenye mtandao wetu. Leo nimechagua kukushirikisha mada inayoitwa “HAKUNA LISILOWEZEKANA” na nikushukuru tu kwa muda wako unaotenga kuendelea kufuatilia makala zetu. Nathamini sana mchango wako huo.

 Zamani niliwahi kuishi mjini Mtwara na kwa kawaida mimi na mke wangu tulikuwa tunaamka saa 10:30 alfajiri ili kujiandaa na kumpeleka mwenzangu kwenye kituo cha busi katika eneo linaloitwa Mnarani wenyeji wa mji wa Mtwara wanajua; kwa ajili ya kuwahi gari la wafanya kazi wa uwanja wa ndege ambako yeye ni miongoni mwa wafanya biashara wachache waliokuwa wanaotoa huduma kwa wasafiri pale uwanjani.

Majira ya saa 11 tayari tulikuwa njiani kuelekea kituoni huku kukiwa na mvua za rasharasha ambazo kwa aina ya usafiri wa pikipiki tunaotumia inatuwia taabu kidogo kutembea huku tunalowa na mvua.Si unajua mvua hata ikiwa kidogo kwa usafiri wa pikipiki ni kama vile unapita ukiikusanya!

Namfikisha katika kituo na wakati anaendelea kusubiri kitambo cha kama dakika tano hivi anatafuta simu kuangalia saa lakini bahati mbaya anagundua kumbe hakuna simu hata moja aliyochukua miongoni mwa simu zake mbili zote alikuwa amezisahau nyumbani. Namshauri pengine nikimbie mara moja nyumbani ili kumletea simu zake kabla ya usafiri wake kufika ananiambia kuwa haiwezekani kwani punde tu gari lilikuwa jirani sana kufika na hivyo singeweza kuwahi.

Upande mmoja wa moyo wangu unasema basi ni jambo haliwezekani lakini upande wa pili wa moyo wangu huo huo unanisukuma kuwa haiwezekani kutokuwezekana kumletea simu zake kwa njia moja au nyingine. Moyoni mwangu Napata aina fulani ya msukumo kuuamini upande wa pili.

Kabla hatujaachana ananipa maagizo na kazi za kufanya ambazo angepaswa kuzifanya kama hangesahau simu zake na hapo tunaachana makubalianao ikiwa ni basi hapakuwa na jinsi atalazima kwa muda wa saa 2 mpaka 3 kutokuwa na mawasiliano hivyo nimsaidie kupokea simu zake kama kungekuwa na mtu ambaye angepiga kabla hajarudi.

Naondoka lakini moyoni mwangu nimekubaliana naye kutokukubaliana huku nikiona kana kwamba kuna njia naweza kufanya kuwahisha simu zake kabla hajachukuliwa na gari pale kituoni. Naazimia kurudi nyumbani kwa kasi kwa ajili ya kufuata simu za mke wangu huku nikiamini nitamkuta bado yuko kituoni.

Kitambo cha dakika kama 5 hivi nafanikiwa kufika nyumbani kuchukua zile simu na kufika kituoni lakini bahati mbaya tayari gari lilikwishapita na kumchukua hakuwepo kituoni.Najilaumu kidogo kwa kuchelewa kuchukua maamuzi kwani muda ambao nilitumia naye kituoni kwa ajili ya kujadiliana inawezekana au haiwezekani ningeutumia kukimbia mara moja ningemuwahi.

Wakati mwingine sumu ya mafanikio yetu inaweza kuwa ni hali ya kushindwa kusikiliza nafsi yako inachosema na badala yake tunasikiliza sauti za nje ambazo mara nyingi huwa haziko sahihi na kujikuta tunashindwa kuchukua maamuzi haraka kwa mambo ambayo hayahitaji kusubiri.

Bado moyoni mwangu sikuwa nashuhudiwa kushindwa na kwa kuwa kulikuwepo na kitu kilichokuwa kinanisukuma yaani sikukubali kushindwa mapema. Wazo likanijia nikajitege katika kituo cha Magomeni ambapo baada ya mzunguko wa kuwachukua wafanyakazi wote katika vituo vyao huwa ni lazima gari lile lipite pale. Nagundua pikipiki yangu haikuwa na mafuta ya kutosha lakini nalimaliza tatizo hilo kwa kujaza mafuta kwani bahati nzuri nilikuwa jirani kabisa na kituo cha mafuta.

Naanza safari kwenda kituo cha Magomeni huku nikiuona uwezekano wa kumpata mtu ambaye anapandia kituo kile ili nimpe simu za mke wangu ampe, hiyo ikiwa ni mpango A na huku mpango B ikiwa ni kusubiri gari ikifika niisimamishe.

Nafika katika kituo na kwa bahati mbaya si kwamba tu hakuna ninayemfahamu lakini hakukuwa kabisa na mtu yeyote. Bado moyoni mwangu nilikluwa naendelea kushuhudiwa kuwa kulikuwa njia.

Nachagua kuvuta subira kidogo huku nikijiuliza hata nikimpata mtu nitawezaje kumpa simu za mke wangu mtu ambaye simjui wala hanijui.Nilihofia usalama wa simu pengine zikapotea lakini moyoni  mwangu bado nilikuwa naona kuna njia.

Kitambo cha dakika kama 5 hivi anatokea mtu ambaye sijawahi kumwona na yeye nina uhakika alikuwa hanijui. Moyoni mwangu naanza kuamini kuwa yule ndg lazima atakuwa ni miongoni mwa wafanya kazi wa uwanja wa ndege wa Mtwara.Si hivyo tu moyoni mwangu nahisi kumwamini pasipo mashaka kwani alikuwa amevaa nguo za walinzi wa moja ya kampuni za ulinzi na moja ya sifa anayopaswa kuwa nayo mtu wa aina hiyo ni uaminifu.

Nakata shauri kuwa nitampa yeye simu huku nikijipa moyo kuwa kwa aina ya kazi yake hata akiamua kutokufikisha wapelelezi kwa maelezo nitakayowapa hawatakuwa na kazi kubwa ya kufanya itakuwa rahisi kumpata na kumkamata.

“Habari za asubuhi mzee” Namsalimia naye anajibu bila kunitilia maanani sana “nzuri” huku akiendelea kushughulika na simu yake.

“Samahani,unafanya kazi uwanja wa ndege?

Yeye: Ndiyo

Mimi: Namsogelea na kuanza kumwomba. Samahani ninaomba msaada wako,mke wangu anafanya biashara pale uwanja wa ndege sasa amesahau simu zake nahisi itakuwa ngumu sana kwake kwa habari ya mawasiliano naomba unisadie kumpa hizi simu utakapopanda kwenye gari”

Yeye:Unaitwa nani na mke wako anafanya biashara gani pale? Nikamwambia na kisha akapokea zile simu za mke wangu na kuahidi kuwa hizo zimefika.Namshukuru nakupanda pikipiki yangu kurudi nyumbani ndani ya dakika kama 20 hivi nafanikiwa kupata suluhu ya changamoto ambayo ilikuwa imeonekana kama vile haiwezekani kabisa lakini imewezekana.

MIMI NA WEWE TUNAJIFUNZA NINI?

Kushindwa au kushinda mara zote ni matokeo ya ndani ya mitazamo yetu. Kile unachoamini kuwa ndicho kitakuwa. Kama ningemsikiliza mke wangu hakika haingewezekana kabisa kuweza kumpelekea simu zake na hakika ningekuwa na kazi kubwa kufanya kazi zake ambazo singefanya kwa ufanisi kama yeye kutokana na ukweli kwamba sina uzoefu kama yeye.

Hakuna changamoto ambayo inakuja kwa ajili ya kutuangusha ila zinakuja kwa ajili ya kutuinua kutoka hatua moja kwenda nyingine na ktufanya kuwa watu bora zaidi ya tulivyokuwa kabla. Kile unachowaza na kukitengenezea msimamo ndicho utakachoishi huwezi kwenda mbali zaidi ya mtazamo wako.

Akili zetu kwa asili zimeumbwa kwa namna ya kuimarika na kupata majibu yaliyotukuka zinapokutana na kiwango cha juu cha changamoto. Upo uwezo hauwezi kuwa tayari kwa ajili yako mpaka tu umefika katika hatua ya kukabiliana na kile ambacho wengine wanaweza kuita kikwazo.

Nataka kumaliza kwa kukuuliza maswali machache hapa. Je wewe ni miongoni mwa watu ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kwa kuruhusu vikwazo kuwa sababu ya ndoto zao kufa? Au je wewe ni miongoni mwa watu ambao wameinyima akili fursa ya kutoa majibu ya maswali magumu ya maisha? Narudia tena kusema hakuna lisilowezekana.

Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala kitu kingine kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini.Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno au whatsapp au piga simu au email tutapokea na kurudi kwako mapema kadri itakavyowezekana.

Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale

Simu +255784503076 

Email:maishanifursa2017@gmail.com

Previous
Previous

Mambo 4 Ya Kufanya Ukipatwa Na Janga.

Next
Next

Alianza Kinyonge Akamaliza kwa Ushindi!