Mambo 4 Ya Kufanya Ukipatwa Na Janga.
Umewahi kupatwa au kukutana na jambo au janga lolote maishani? Au kama siyo wewe labda umewahi kumwona mtu ambaye amefikwa na janga kubwa? Ingawa majanga yanatofautiana kwa ukubwa binadamu wengi wamewahi kukutana au kufikwa na janga kubwa au dogo.
Janga ni kitu au hali yoyote ambayo huna uwezo wa kuizuia inayotokea ghafla bila kutarajia wala kutegemea. Inaweza kuwa ulivamiwa na mafuriko,kupata hasara kubwa katika biashara,kufukuzwa kazi,nyumba au biashara yako kuungua moto,kuvamiwa na majambazi au kukataliwa na mpenzi wako ghafla n.k.
Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “MAMBO 4 YA KUFANYA UNAPOKUTANA NA JANGA.” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana.
Haya yote pamoja na mengine ambayo hayakupata nafasi ya kuoorodheshwa hapo juu ni mambo ambayo hayatarajiwi na ukweli kama ungepewa nafasi ya kuchagua hakuna binadamu ambaye angekuwa radhi kuchagua majanga.
Huwezi kwa mfano kuzuia mafuriko,kimbunga,moto,ajali au kuzuia kukataliwa ghafla na mpenzi ambaye hukutegemea kabisa. Iwe unataka au hutaki mambo haya lazima yatatokea na uwezo wa kuzuia huna kwa sababu yako nje ya uwezo wa mwanadamu.
Kwa kuwa ni hali ambayo iko nje ya uwezo wa binadamu kuweza kuzuia isitokee, kwa hali hiyo wakati wa kupokea au kushuhudia janga unatakiwa kuwa mwangalifu sana kwani kuna fursa ya kufanya maamuzi ambayo yataathiri maisha yako yote kwa namna chanya au hasi.
Kila dakika inayopita kwa kujua au hata bila kujua binadamu tunafanya maamuzi makubwa na madogo ambayo yana uwezo wa kuathiri maisha yetu kwa namna moja au nyingine.Cha muhimu kukumbuka tu ni kwamba uamuzi wowote utakaochukua bila kujali umepita katika hali gani mbele kuna matokeo.
Sasa unapokutana na hali ya namna hii unapaswa kufanya nini ili maisha yaendelee kama kawaida? Hapa kuna mambo 4 kwa ajili ya kukusaidia:-
WEWE SIYO WA KWANZA
Hakuna jambo litatokea ambalo halijawahi kutokea kwa mwingine. Wewe huwezi kuwa ni wa kwanza kuna mlolongo wa watu ambao walishatokewa na jambo unalopitia na wanaendelea kuishi. Ni ajabu kwa sababu kwako linatokea kwa mara ya kwanza lakini siyo ajabu kwa watu wote. Ukishajua kuwa wewe siyo wa kwanza itakusaidia kufikiri vizuri na kufanya maamuzi sahihi.
Janga ni swala la msimu na msimu huwa siyo kitu cha kudumu kinakuwepo kitambo kidogo halafu kinapita.Ukishajua hivyo hakuna busara yoyote kufanya uamuzi wa kudumu ambao utaathiri maisha yako kwa kutegemea tu mhemuko unaotokana na janga unalopitia.
POKEA JINSI YALIVYO
Kitu kilichotokea kiko nje ya uwezo wako kuzuia! lah ungeweza hungeruhusu hata kidogo kikatokea. Kwa kuwa hali iko hivyo basi hatua ya kwanza unayotakiwa kufanya ili uweze kubaki katika namna ambayo una nguvu ya kuendelea ni kukubali na kupokea matokeo kama yalivyo.
JIULIZE HUU NI MWANZO AU MWISHO?
Umewahi kujiuliza ni kitu gani kinachopelekea mtu akipatwa na janga anafanya maamuzi magumu na mwingine kufanya maamuzi ambayo yatafanya awe mtu wa kutiliwa mfano kila siku? Tafsiri ambayo mtu anatoa pale anapokutana na jambo lolote ambalo hakulitegemea katika maisha kumtokea ndiyo inayopelekea mtu kufanya maamuzi ya busara au ya hovyo!
Ndiyo maana unakuta mtu mmoja kwa kukataliwa na mpenzi wake anaamua kujinyoga na mwingine anapokutana na hali ya namna hiyo anaamua kutulia na mwisho wa siku anapata mtu anayempenda hata zaidi ya yule aliyemkataa.
Tofauti ya watu hawa wawili ni tafsiri siyo kingine. Huyu aliyekataliwa na kuamua kujinyonga ametafsiri kwamba huo ndiyo mwisho wa kupenda na kupendwa kamwe hatakaa ampate mtu atakayempenda kama yule. Lakini huyu wa pili anauona huo kuwa ni mwisho wa penzi lake na mpenzi aliyeamua kumkataa lakini kwa upande mwingine huo ni mwanzo wa safari nyingine mpya kumsaka mpenzi sahihi watakayevumiliana wakati wa shida na raha.
Mchungaji Chriss wa nchini Afrika kusini katika mafundisho yake aliwahi kusema “ukiona tatizo linatokea basi tayari na njia ya kulitatua ipo” Kwa lugha nyingine tatizo haliwezi kutokea kama njia haijawa tayari. Kwa hiyo unachotakiwa kufanya pale unapokutana na janga jipe nafasi ya kujiuliza vizuri swali la kwanza “Je nini maana yake hii?” swali la pili “Je huu ni mwisho au mwazo mpya?” Kwa jinisi akili ya mwanadamu ilivyo itakuonyesha kuwa ni mwanzo mpya unapaswa kujipanga na kusonga mbele maisha bado yapo.
ANZA UPYA TENA
Ulichopitia ni uzoefu ambao watu wengi hawajawahi kuupata. Katika maisha yako utakutana na watu wengi sana ambao wanahangaika kwa kuwa wanapitia katika msimu ambao ni mara yao ya kwanza kupitia. Badala ya kukaa na kuendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu juu ya janga ulilopitia na mahali lilipokufikisha,unapaswa kusahau yaliyopita na kuanza mwanzo mpya. Unapaswa kuanza upya huku ukiwa na tahadhari ukijitahidi kadri utakavyoweza kuepuka kukosea sana.
Haijalishi unapitia au umepitia katika hali gani mafanikio yapo mlangoni yanakusubiri uamue kufanya kitu yajivute kuja kwako. Hakuna jambo linatomtokea mtu ambalo Mungu hajaweka kusudi la kukusaidia kupitia hali au janga unalopitia. Itategemea tu unavyofikiri na kuamua.
Kwa kuwa akili yako utakuwa umeielekeza kukubaliana na ukweli kwamba janga ni kitu cha msimu siyo kitu cha kudumu na kupokea matokeo jinsi yalivyo,na kwa kuwa umeamua kujiuliza maswali ya nguvu na kuanza upya;hakuna sababu itakaayokuzuia kuanza safari mpya ya mafanikio. Kipindi ulichopitia kinaweza kubaki kuwa historian a uzoefu wa kusaidia watu wengine.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu:+255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com