William Kamkwamba-Kutoka Umasikini Hadi Utajiri.
Kutoka Kuzaliwa Katika familia masikini leo William Kamkwamba ni mhandisi mwenye mafanikio makubbwa
Hakutazama hali ya umaskini uliokuwa unamzunguka yeye na familia yake na kukataa kutumia hali hiyo kama kikwazo cha kuishi maono yake, zaidi ya kuangalia ni namna gani angeweza kutumia kitu pekee ambacho Mungu amempa ambacho ni kipaji na ubunifu kujikwamua yeye,familia na jamii inayomzunguka kutoka kwenye lindi la umasikini.
Karibu tena msomaji wetu wa mtandao huu wa maisha ni fursa. Leo tutajikita zaidi kwenye mada ambayo nimeipa kichwa “JIFUNZE KUTOKA SHUJAA KAMKWAMBA.” Nashukuru kwa kuendelea kutuamini na kufuatilia kazi zetu,kwani bila wewe kazi yetu haina maana
Ni mbunifu,mhandisi na mtunzi wa vitabu,aliyezaliwa mwaka 1987 kutoka katika familia maskini nchini Malawi,familia ambayo haikuwa na uwezo hata wa kuwapa watoto baadhi ya mahitaji muhimu ya maisha.
Kutokana na hali ya umaskini uliopitiliza wa familia yake,William Kamkwamba alikatisha masomo yake akiwa na umri wa miaka 14 baada ya wazazi wake kushindwa kumlipia shs kama laki moja na elfu 70 za kitanzania kugaharamia masomo yake kwa mwaka.
Kamkwamba hakutazama hali ya umaskini uliokuwa unamzunguka yeye na familia yake,ila aliangalia ni namna gani anaweza kutumia kitu pekee ambacho Mungu amempa ambacho ni kipaji na ubunifu kujikwamua yeye na jamii inayomzunguka.
Kabla hajapata mafunzo yoyote ya namna ya kutambua fursa za biashara alijua bila kufundishwa na mtu yeyote kuwa wazo la biashara chanzo chake ni matatizo yaliyo katika jamii fulani.
Alijiuliza ni matatizo gani ambayo yapo katika kijiji chake na kugundua kuwa moja ya tatizo kubwa ambalo lilikuwa linachangia ongezeko la umaskini katika kijiji chao ilikuwa ni kutokuwepo kabisa nishati ya umeme
Kwanza alijitofautisha na vijana wengine pale kijijini ambao walikuwa wanalalamikia tu namna ambavyo serikali au wafadhili walikuwa wamesahau kijiji chao kwa kutokukiweka katika mpango wa kupatiwa umeme.
Alichukulia hiyo hali kama fursa badala ya tatizo kama wanakijiji wengine walivyokuwa wanaamini. Kwa kubadili tu alivyokuwa anafikiri kuhusiana na changamoto ya kutokuwepo umeme kijijini kwao alianza kuona uwezekano wa kufanya jambo na hangehitaji mtu mwingine kufanya zaidi yake.
Alianza kufikiri nje ya boksi ni namna gani yeye anaweza kufanya kusaidia kijiji chao kuondokana na tatizo la muda mrefu la nishati.Kwa kuanza kujielekeza katika kutafuta suluhu alijikuta mazingira yanayomzunguka yanaanza kumpa kila aina ya msaada aliohitaji,kufanikisha azma yake.
Aligundua moja ya vitu vilivyokuwepo kwa wingi katika kijiji chake na maeneo mengine ni pamoja na upepo ambao haukuwa na matumizi yoyote,hivyo alianza kutafuta njia ya kutumia upepo kufua umeme kwa ajili ya mahitaji ya kijiji chao.
Kutokuwa na ujuzi na maarifa ya kutosha juu ya kile alichotaka kufanya haikuwa sababu ya kumfanya asubiri mpaka atakapopata mfadhili kumpeleka chuoni kusomea maswala hayo,Kwa kifupi alichagua kuanza kutumia kile alichonacho badala ya kuhangaika kutumia kile asichonacho.
Alijuliza ni kitu gani ambacho kilikuwa ndani ya uwezo wake ambacho kingemwezesha kuanza kutekeleza ndoto yake kabla ya kuhitaji kusaidiwa na watu wengine? Alifanya tathmini na kugundua alikuwa na uwezo mwingi ndani mwake mwenyewe kumwezesha kuanza safari ya kukiondoa kijiji chake katika giza.
Kwa kuwa alikuwa amejifunza kusoma na kuandika alianza kutumia muda wake kujisomea vitabu na machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kuhusiana na maswala ya umeme wa na mwisho alifanikiwa kupata namna ya kutengeneza chombo cha kufua umeme kutokana na upepo.
Wakati wote akifanya majaribio watu walimuuliza alichokuwa anahangaika kufanya walimcheka sana pale alipowaambia kwamba alikuwa anatengeneza kifaa cha kufua umeme kwa kutumia upepo ili kuondoa tatizo la nishati kijijini kwako hawakumwamini kabisa zaidi ya kumowna kama mtu aliyechanganyikiwa.
Penye nia pana njia Kamkwamba alifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliweza kufua umeme kwa kutumia upepo na kuacha watu wengi vinywa wazi hata wale waliokuwa hawaamini alichokuwa anasema.
Habari ya Kamkwamba kuwa mtu maarufu kutokana na uvumbuzi wake wa kuzalisha umeme kutokana kwa nguvu ya upepo zilianza kuvuta hisia za watu wengi kijijini,nchini na hata nje ya nchi.Mwanzo wa Kamkwamba kujulikana duniani ilikuwa ni pale shirika la utangazaji la uingereza BBC lilipata habari ya kuwepo kwake na kutengeneza makala maalumu kwa ajili ya kijana mdogo toka nchini Malawi William Kamkwamba na ubunifu wake.
Hatimaye Kamkwamba alipata fursa ya kulipiwa gharama kwenda nchini Marekani kuzungumza kwenye jukwaa maarufu la TED. Kutoka kijijini nchini Malawi hadi kualikwa nchini Marekani kuzungumza mahali ambao wanenaji wenye kitu cha pekee kutoka duniani kote hupata nafasi ya kuzungumza mbele ya watu wengi maarufu duniani unaowasikia.Hapo alizungumza kuhusu ubunifu wake wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya upepo hatua ambayo alifanya bila kuwa na pesa.
Kuanzia hapo nyota ya William Kamkwamba ilianza kung'ara,alipata watu wa kusaidia kuboresha na kukuza wazo lake sambamba na kumpa ufadhili kusomea maswa la ya umeme hadi hatua ya shahada ya chuo kikuu. Leo Kamkwamba ni miongoni mwa watu maarufu barani Afrika wa kutolea mfano aliyefanikiwa kutoka umaskini wa kupindukia hadi kuwa mtu aliyeleta neema nchini mwake kwa kugundua namna ya kufua umeme kwa kutumia nguvu ya upepo.
Wakati anatafuta namna ya kufua umeme kwa kutumia upepo hata wazazi wake waliona kama anataka kuchanganyikiwa kwa kuwaza mambo yasiyowezekana na wana kijiji walimchukulia kama mtu aliyekuwa anavuta bangi,hakukata tamaa hata kidogo.
KUNA FUNZO GANI HAPA?
Mara nyingi watu wameshindwa kuanza kuishi ndoto zao kwa kusingizia kuwa hawana pesa ya kuanzia na kusahau kuwa pesa ni hitaji moja kati ya mengi kukuwezesha kuishi ndoto yako. Kwa mtindo huu watu wengi wamekufa na mawazo ya thamani kabla hata ya kuanza kuitendea haki dunia hii.
Ukweli ni kwamba wakati mwingine Mungu amezuia baraka tele kwetu kwa kuwa tu watu wengi hawana uwezo wa kuona thamani ya kitu kidogo cha thamani walicho nacho. Kama huna uwezo wa kutumia kitu kidogo Mungu alichoweka ndani mwako kwa nini akudhamini kwa kitu kikubwa?
Kabla hujalalamika juu yale mambo ambayo unaona yanapungua na kuwa vikwazo kwako kufanya maendeleo unapaswa kuthamni na kutumia kidogo Mungu alichokudhaminisha kama njia ya kuvuta baraka kubwa zaidi.
Mambo hayo yaweza kuwa ni fedha kidogo unayoona haitoshi hakuna fedha ndogo wala kubwa.Inaweza kuwa ni kipaji ambacho Mungu amekupa toka nje kitumie utaona namna watu watakavyojitokeza kuunga mkono kwenye kazi yako. Yaweza kuwa chochote unachoweza kusema hebu jiweke katika mazingira ya kuthamni kilichoko mkononi mwako kabla ya kutamani mambo makubwa.
Watu wengi wanatamani kusaidia watu wanaojaribu kufanya kulingana na uwezo na nguvu waliyo nayo badala ya wale wanaopenda ksuema sana jinsi ambavyo wanaweza kufanya lakini hawana uwezp wakimaanisha pesa.
Pes halijawahi kuwa tatizoa la msingi kukwamisha mtu alifanye anachotaka kufanya.Kama ingekuwa hivyo Kamkwamba leo angekwisha jiunga na mlolongo wa familia yake na kutengeneza ukoo wa maskini zaidi lakini yeye alikataa pamoja na ukweli kwamba alikuwa hana pesa kabisa.
Maisha ni fursa bila mipaka,kule kuwa hai tu ni fursa muhimu kukuwezesha kufanya,au kuwa chochote unachotaka kuwa.Haijalishi umezaliwa katika mazingira na hali ya namna gani,ili mradi Mungu amekupa zawadi ya kipaji na ubunifu unao uwezo wa kutoka katika hali uliyo nayo na kubadilisha kabisa historia ya maisha yako na watu wanaokuzunguka.
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote au ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasiliana nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Simu:+255784503076
Email:maishanifursa2017@gmail.com