Ujinga Siyo Kitu Kibaya tu!
Siyo Lazima Ujinga Kuwa kitu Kibaya
Ingawa ujinga siyo lazima kuwa kitu kibaya,katika hali ya kawaida hakuna mtu ambaye angependa kuitwa mjinga.Umewahi kuona watu wakigombana na amani kuvurugika kwa kuwa tu mmoja amemwita mwenzake mjinga?
Watu wengi kwa kujua au hata bila kujua hujikuta wanaingia kwenye ugomvi mkubwa kwa kuwa tu mtu fulani amewaita wajinga wakati wao wenyewe wanajiona siyo wajinga.Uwe mwangalifu kwa sababu binadamu wote jinsi tulivyo hata yule unayemhesabu kuwa mwerevu sana anayo aina fulani ya ujinga.
Kinachotofautisha tu watu wengi sasa ni namna ya kuushughulikia huo ujinga; kuna ambao wanajua wanaukumbatia ujinga na kuandaa makazi kwao na wale ambao kamwe wakigundua kuwa ni wajinga katika eneo fulani basi wanatafuta dawa ili wapone. Tafsiri nyepesi tu ujinga ni ile hali ya kutokujua kitu na kama inakaa hivyo basi kuna ubaya gani kama mtu hajui kitu fulani kwani lazima mtu atimie katika kila idara maishani mwake? Hapana.
Hebu fikiri mtu mmoja anakuambia wewe hujui,au huelewi na mwingine anakwambia wewe mjinga tafsiri ya maneno hayo yaweza kuwa inakaribiana sana yaani ni mjinga kwa kuwa lipo eneo ambalo huna ufahamu nalo.
Kwa uzoefu wangu kuna ujinga wa aina mbili: kwanza ni ule ujinga wenye manufaa na ujinga usiokuwa na manufaa yoyote kwa mtu aliyeubeba. Kutokana na hali hiyo tunapaswa kuwa waangalifu sana tunaposhughulikia matokeo yanaoletwa na tafsiri zetu za ujinga.
Ukweli ni kwamba huhitaji kukasirika kabla ya kujiridhisha kama aliyekuita mjinga amekuweka kwenye kundi la wajinga waliobeba ujinga wenye manufaa au miongoni mwa wale waliobeba ujinga usio na manufaa yoyote!
Kuna msemo uliozoeleka sana katika jamii, ambapo utasikia watu wakisema “afadhali ya ujinga kuliko upumbavu” kwa kuwa mjinga hufundishika lakini mpumbavu hata ukimtwanga pamoja na ngano upumbavu hauwezi kutoka ngano itasagika na kuuacha upumbavu.
Mimi pia hainidhuru ukiniita mjinga kuliko ukiniita mpumbavu maana ujinga ni kitu unaweza kuchagua kuishi nacho kikafanya makazi kwako au ukachagua kutokuambatana nacho kabisa kikatoka kwako lakini siyo upumbavu. Hatari kubwa ni pale mtu unapokuwa mjinga lakini hujijui kama ni mjinga matokeo yake utapishana na fursa nyingi za watu kukusaidia kuondokana na ujinga katika eneo fulani ulilokwama.
Kwangu mjinga ni yule anayejua hajui lakini anajifanya anajua na hivyo kukosa fursa ya kujifunza kwa watu wengine wanaojua zaidi yake katika eneo ambalo yeye ni mjinga ili kuufukuza ujinga. Binadamu wote jinsi tulivyo tunao upungufu ambao tunaweza kuuita ujinga katika eneo moja au mawili ambalo tungehitaji kujitambulisha kwa watu wanaoweza kutusaidia mara moja na kuondokana na ujinga katika eneo hilo.
Ujinga usio na manufaa
Ujinga usio na manufaa ni pale mtu ambaye ni mjinga anajua kuwa lipo tatizo mahali fulani haelewi,wakati huo huo mtu huyo hafungui milango ya ufahamu kujifunza kutoka kwa watu wengine.
Utakuta mtu wa aina hii siku zote hataki kushindwa na wala hakubali kama kuna eneo hajui yaani anajihesabia haki kuwa yeye anajua kila kitu.Kutokana na msimamo huo mtu huyo anaishia kufunga kabisa milango ya kujifunza maarifa kutoka kwa watu wengine na ni rahisi sana mtu huyo kufa na ujinga.
Ni rahisi sana mtu huyu kuachwa na watu bila msaada kwa sababu milango ya kujifunza kwake imefungwa kabisa. Anajihesabia kujua hata mambo ambayo yako nje kabisa ya uwezo wa ufahamu wake na msaada unakaa mbali.
2. Ujinga wenye manufaa
Ujinga wenye manufaa ndicho kitu ambapo kimebeba sura ya mjadala huu. Huyu ni yule ambaye hata ukimwita mjinga hawezi kukasirika haraka kwani anajitambua kwamba yeye kama binadamu anayo mapungufu mengi ambayo anapaswa kuyashughulikia ili yapungue kama siyo kwisha.
Mtu wa namna hii yuko tayari kuwa mwanafunzi kwa mtu yeyote bila kujali kama ni mkubwa au mdogo ili mradi akibaini mtu huyo anacho kitu cha kumfundisha ambacho yeye hana,haoni kazi kujishusha na kuwa mwanafunzi wa muda ili afute ujinga katika eneo fulani. Ni rahisi sana mtu wa namna hii kupata msaada kutoka kwa watu wengine kutokana na jinsi alivyojiweka na hawezi kufa na ujinga kwa sababu amejitanabaisha kuwa yeye kuna mahali hajui na anahitaji msaada.
Huu ndio aina ya ujinga ninaouita wenye manufaa kwa kuwa kufanya hivyo hawezi kuendelea kuishi daima kwenye kundi la watu wajinga,ujinga kwake ni kitu cha kupita na ni mlango wa kuvuta maarifa mapya kwani hakuna wakati hata mmoja ambapo itatokea mtu kuwa mjuzi wa kila kitu.
3. Ogopa upumbavu
Kitu unachopaswa kuogopa ni upumbavu. Kwa nini? Hiki ndicho kitu hatari kukiogopa kuliko ujinga. Hata katika neno la Mungu kwenye kitabu cha Mithali 27:22 “hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; upumbavu wake hautamtoka”
Naamini utakuwa umepata kitu kupitia makala hii fupi. Ukiwa na uhitaji wowote wa ushauri katika eneo lolote la kuboresha maisha yako usisite kuwasili nasi kupitia njia za mawasiliano hapo chini. Aidha kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno, whatsapp kupiga simu au kututumia barua pepe nasi tutarudi kwako mapema iwezekanavyo.
Ni mimi rafiki na kocha Philipo Lulale
Barua Pepe: maishanifursa2017@gmail.com
Simu:+255784503076